U.S. Ambassador to the Republic of Tanzania, Michael A. Battle during the presentation of colors by the U.S. Marines at the U.S. embassy’s Fourth of July, Independence Day celebration. |
KATIKA kuadhimisha miaka 248 ya uhuru wa Marekani, tulifanya sherehe kubwa nyumbani kwangu, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania January Makamba alikuwa mgeni rasmi na mamia ya marafiki wa Kitanzania wa Marekani walihudhuria.
Tarehe 4 Julai ni siku ya kuzaliwa kwa Marekani kama tunavyoijua sasa – ni siku ya kutambua na kuenzi ushindi wa kujitawala uliopiganiwa vikali na waasisi wa taifa la Marekani. Siku ya Uhuru wa Marekani ni wakati wa kurusha fataki na fashi fashi, kuchoma nyama na kujumuika pamoja kama jamii, lakini pia ni wakati wa kutafakari juu ya maadili na amali zetu za pamoja – uhuru, demokrasia, na ushiriki wa kiraia.
Uhuru wa kujieleza ni nguzo muhimu ya demokrasia. Inawawezesha watu kutoa maoni yao, kuchangia Mawazo yao, na kuwawajibisha viongozi wao. Nchini Marekani, haki hii ya msingi inathaminiwa na kulindwa, hivyo kuruhusu kuwa na jamii yenye nguvu na yenye kupenda na kuhimili mabadiliko ambapo mitazamo tofauti mbalimbali inaweza kustawi.
Hali kadhalika, nchini Tanzania, sauti za raia ni muhimu katika kuunda mustakabali wa taifa. Kuhimiza mazungumzo ya wazi na kuheshimu mitazamo tofauti kutaimarisha mshikamano wa jamii na kukuza utamaduni wa maelewano na maendeleo. Ni muhimu kutambua kuwa uhuru huu, japokuwa ni wa msingi, si mara zote raia wanahakikishiwa kuupata, hivyo ni lazima utetewe na ulindwe – hususan wakati unapokabiliwa na changamoto mbalimbali duniani kote.
Kama Rais Joe Biden alivyopata kusema, “Demokrasia haitokei tu kama ajali. Tunapaswa kuilinda, kuipigania, kuimarisha na kuihuisha.” Maneno haya yanagusa vizazi vyote vya Wamarekani, tangu wale waliopigana kwa ujasiri kuanzisha taifa huru. Kwa miaka mingi, kupitia enzi ya harakati za kupigania ya haki za kiraia na kuendelea hadi leo, tumekuwa tukipigania kupanua na kuimarisha demokrasia kwa Wamarekani wote.
Tunatambua kuwa kazi ya kujenga demokrasia nchini Marekani, kama ilivyo kwa Tanzania, inaendelea kuwa kazi inayoendelea tunapojitahidi kujenga “muungano mkamilifu zaidi.” Tamanio hili kuu na la kudumu la kuwa watu huru na wanaojiamulia mambo yao wenyewe ndilo lililomhamasisha Mwalimu Julius Nyerere kupigania uhuru wa Tanzania zaidi ya miongo sita iliyopita. Tunaungana na watu wa Tanzania kuunga mkono juhudi za utekelezaji kamili wa maadili yetu ya pamoja ya kidemokrasia.
Kufanya kazi kwa kujitolea ni nguzo nyingine ya jamii yenye afya na inayoshiriki kikamilifu katika masula yanayoihusu. Nchini Marekani, utamaduni wa kujitolea umekita mizizi, ambapo Wamarekani wengi hujitolea muda na ujuzi wao kusaidia wahitaji.
Ninajivunia sana kazi inayofanywa na wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps kwa kushirikiana na jamii za wenyeji wao huko Kilimanjaro, Tanga, Zanzibar na Dodoma. Na ninajivunia zaidi ushirikiano wa timu ya Peace Corps na Wizara ya Afya kuanzisha Mpango wa Kujitolea wa Nchi Mwenyeji (Host Country Volunteerism Program) katika sekta ya afya, unaowaunganisha wafanyakazi wa kujitolea wa Kitanzania na wale wa Peace Corps katika kuleta mabadiliko katika jamii zao.
Kipekee kabisa nimeguswa na jitihada zisizo na ubinafsi za madaktari na wauguzi wa Kimarekani wanaojitolea kuwahudumia Watanzania bila malipo. Watu kama Dk. na Bi. Irving Williams ambao kwa miaka hamsini wamekuwa wakiwaleta watoa huduma za afya na waelimishaji nchini Tanzania kupitia Ahead Inc., shirika lisilo tengeneza faida lililosajiliwa nchini Tanzania, ambalo litarejea mkoani Kagera wiki ijayo na madaktari na wauguzi kutoka jimbo kuu la New York ili kuendesha kliniki maalumu ya afya bila malipo. Shule za sekondari na vyuo vya Marekani vinazidi kujitolea kudhamini mafunzo ya utoaji huduma nchini Tanzania.
Vijana hawa na wataalamu wanaonyesha roho ya kujitoa, kujitolea na huruma, wakithibitisha kuwa huduma ya kweli haina mipaka. Kazi yao haiboresha tu afya ya jamii wanazozihudumia bali pia hujenga madaraja ya urafiki na ushirikiano kati ya mataifa yetu.
Ushiriki kamilifu wa raia ni muhimu sana katika kulinda na kuendeleza demokrasia. Raia wanaoshiriki kikamilifu ni roho ya demokrasia, wakishiriki katika mchakato wa uchaguzi, kutetea jamii zao, na kuhakikisha kwamba serikali zao zinawajibika kikamilifu na kuendeshwa kwa uwazi. Nchini Marekani na hata Tanzania, raia wanaoshiriki kikamilifu wana nafasi na jukumu muhimu la kulinda maadili ya kidemokrasia na kukuza haki za kijamii.
Tunapoingia kipindi muhimu cha uchaguzi mwishoni mwa mwaka huu katika nchi zote mbili, ni muhimu kwamba raia wachukue jukumu hili kwa uzito unaostahili, na washiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi wa kesho. Hii si muhimu tu katika uchaguzi wa urais, bali ni muhimu pia, ikiwa sio zaidi, katika ngazi ya mitaa, ambapo viongozi waliochaguliwa wanajukumu kubwa katika kuboresha maisha ya raia wa kawaida.
Tunaposherehekea Siku hii ya Uhuru wa Marekani, ninawahimiza Watanzania wote kuzingatia na kuheshimu uhuru wa kujieleza, kujitolea, na ushiriki kamilifu wa kiraia. Kwa kufanya hivyo, mtakuwa mnachangia katika kuliimarisha na kulipa uhai taifa lenu, mkihakikisha kwamba demokrasia inastawi na kwamba sauti za raia wote zinasikika na kuheshimiwa. Pamoja, kwa kuheshimiana, kuelewana na kushirikiana, tunaweza kujenga mustakabali mzuri kwa wote.
Heri ya Uhuru wa Marekani!
Balozi Michael Battle
No comments:
Post a Comment