BENKI ya NMB imetoa gawio la Tsh. Bilioni 57.4 kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni kiashiria cha azma ya kuleta tija na faida kubwa kwa wawekezaji wao wote, ikiwemo Serikali yenye umiliki wa 31.8% katika Benki yetu.
Kwa mwaka huu, hili ni Gawio kubwa zaidi kutolewa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka taasisi za kibiashara ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepokea mfano wa hundi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NMB - Dkt. Edwin Mhede pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB – Bi. Ruth Zaipuna katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna alisema: “Kutokana na mazingira wezeshi na uimara wa sekta ya kibenki, NMB ni miongoni mwa mabenki yaliyokua sana. Gawio la jumla limeongezeka kutoka Tsh bilioni 97 mwaka 2021, hadi kufikia bilioni 181 mwaka 2023. Gawio kwa Serikali limeongezeka kutoka Tsh 30.8bn mwaka 2021 hadi kufikia Tsh 57.4bn mwaka 2023.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia ameipongeza Benki ya NMB kwa matokeo mazuri ya kiutendaji yaliyopelekea kuongezeka kwa faida kwa taasisi na gawio kwa Serikali.
Wakati wa hafla hiyo, Rais Samia pia aliikabidhi tuzo Benki ya NMB kutambua mchango wao katika kutoa gawio kubwa kwa Serikali mwaka hadi mwaka.
“Tunawashukuru wadau wetu wote kwa kuwa sehemu ya mafanikio haya,” alimalizia Bi. Zaipuna.
#NMBKaribuYako
No comments:
Post a Comment