TMA YATOA MWELEKEO MVUA ZA MASIKA KUANZIA MACHI HADI MEI, 2025....! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 23 January 2025

TMA YATOA MWELEKEO MVUA ZA MASIKA KUANZIA MACHI HADI MEI, 2025....!

Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chan’ga na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa utabiri.

Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chan’ga na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa utabiri.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za masika kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, huku ikibainisha uwepo wa mvua za wastani hadi Chini ya Wastani katika maeneo ya pwani ya kaskazini yanayojumuisha mikoa ya Morogoro, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi Dkt. Ladislaus Chan’ga amesema hali hiyo itajiri pia kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na ukanda wa Ziwa Victoria ikijumuisha Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara.

Aidha, alisema Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani pia zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu, huku zikitarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi, 2025 katika maeneo ya kanda ya Ziwa Victoria na pwani ya kaskazini; na wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi,  2025 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki.

"...Ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Aprili, 2025. Athari zinazotarajiwa: Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani. Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka hivyo kuongeza hatari ya mafuriko hususan katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko," alisisitiza Dkt. Chan’ga katika taarifa yake ya utabiri.

Hata hivyo alibainisha upo uwezekano wa Magonjwa ya mlipuko kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji, hivyo kuzitaka mamlaka husika kujipanga kukabiliana na hali hiyo itakapojitokeza.

Pamoja na hayo, Dkt. Chan’ga ameongeza kuwa Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo zinaweza kusababisha upungufu wa upatikanaji wa maji kwa matumizi ya majumbani, kilimo na ufugaji. Hivyo, Mamlaka za miji na wilaya zinashauriwa kuchukua hatua madhubuti ikiwemo kuimarisha na kuboresha mifumo ya usambazaji maji safi ili kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa maji katika kaya na sekta nyingine. 

"Waandishi wa Habari wanashauriwa kufuatilia na kupata taarifa sahihi za utabiri wa Hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kutoa taarifa kwa wakati kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu athari zinazoweza kujitokeza. Wanahabari wanashauriwa kutafuta na kutumia ushauri wa kisekta kutoka kwa wataalam wa sekta husika ili kuandaa na kusambaza makala na ripoti za kisekta kwa lugha rahisi kwa lengo la kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu matumizi sahihi ya utabiri wa hali ya hewa katika kukabiliana na athari zinazotarajiwa."

No comments:

Post a Comment