Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
SERIKALI imeinyang'anya Manispaa ya Ilala, mkoani Dar es Salaam shilingi bilioni 3 ilizoipatia kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Kimkakati wa Machinjio ya Kisasa wa Vingunguti, baada ya Manispaa hiyo kushindwa kutekeleza kwa wakati mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 8.5.
Hatua hiyo imechukuliwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo wa Kimkakati katika Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa Serikali ilitoa kiasi cha Sh. bilioni 3 kati ya Sh. bilioni 8.5 za kukamilisha mradi wa Machinjio ya Vingukuti kuanzia mwezi Mei, 2018, chakushangaza hadi sasa fedha hizo hazijatumika hata senti moja.
"Fedha haziwezi kukaa kwa mwaka mzima bila matumizi ilihali kuna maeneo mengine ambako fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, hivyo tunazichukua fedha hizi na Manispaa ya Ilala mtalazimika kuomba upya mtakapokuwa mmejipanga" Alieleza Dk. Kijaji.
Alibainisha kuwa kwa mujibu wa taratibu za fedha za Serikali zinazopelekwa kwenye miradi zinatakiwa zianze kutumika ndani ya miezi mitatu lakini Manispaa ya Ilala haijazitumia fedha hizo huku karibu Mwaka wa Fedha ukikaribia kumalizika.
"Tunaiangusha dhamira njema ya Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli ya kuwahudumia Watanzania waliosubiri kuhudumiwa kwa upeekee ndo maana tukaanzisha miradi hii ya kimkakati ya kuongeza mapatio ya halmashauri na mkaleta maandiko yenu Serikali ikatoa fedha kumbe hamko tayari na mnatukwamisha kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi," alisema.
"Tumewapatia fedha Mmeshindwa!, kwahiyo wana Ilala na WanaVingunguti, kwamba Serikali yao ina dhamira njema lakini wapo watu wanaotuangusha kwahiyo tutazichukua fedha hizi mpaka hapo Manispaa ya Ilala watakapo leta mpango kazi unaotekelezeka na siyo huu ambao hawakujiandaa" alisisitiza Dk. Kijaji.
Dk. Kijaji alisema kuwa kabla ya kuomba fedha za miradi ya kimkakati ni lazima masuala yote ya upembuzi yakinifu yawe yamefanyika na kama hayakufanyika basi Manispaa ilimdanganya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wazifri wa Fedha ambaye aliridhia Manispaa ya Ilala ipewe fedha hizo.
Naye Naibu Kamishna wa Bajeti wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Charles Mwamwaja, alieleza kuwa Manispaa ya Ilala, imekiuka mkataba ama makubaliano ya kupewa ruzuku ya sh. bil 8.5 kwa ajili ya mradi huo na ni lazima sheria ya fedha ichukue mkondo wake kwa uzirejesha fedha hizo kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina hadi hapo watakapo kuwa tayari.
"Mhe. Naibu Waziri, kuna dosari kubwa katika utekelezaji wa mradi huu na kwa kuzingatia malengo ya miradi kama hii tukienda namna hii, hatuwezi kufanikiwa, sisi tulidhani walipoleta maombi ya mradi huu walikuwa wamejiandaa kumbe sivyo" aliongeza Dk. Mwamwaja.
Kwa upande wake Afisa Mipango wa Manispaa ya Ilala Bw. Ando Mwankuga, alikiri kuwa kulikuwa na ucheleweshaji wa kuanza kutekeleza mradi huo kwa kile alichodai ni kuchelewa kwa mchakato wa kufanya ununuzi na mabadiliko ya mara kwa mara ya kiufundi kutoka kwa mtaalam mshauri wa mradi huo.
"Ucheleweshaji huu si wa makusudi bali ilikuwa ni kuhakikisha tunafuata taratibu zote za ununuzi na kuhakikisha kuwa mradi utakaojengwa uwe na ubora unaotakiwa na unaolingana na thamani ya fedha na tunatarajia kuanza kuutekeleza Machi 10, 2019" aliongeza Bw. Mwankuga.
Manisapaa ya Ilala, ilikuwa miongoni mwa Halmashauri na Manispaa 17 nchini zilizopatiwa ruzuku na Serikali kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 147 katika awamu ya kwanza katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati itakayochochea upatikanaji wa mapato ya ndani na kuzijengea uwezo Serikali hizo za Mitaa na miradi hiyo inatakiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18 kuanzi Mwezi Mei, 2018.
No comments:
Post a Comment