NMB YAWA TAASISI YA KWANZA YA KITANZANIA KUTAMBULIWA KAMA MWAJIRI KINARA NA TOP EMPLOYERS - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 16 January 2025

NMB YAWA TAASISI YA KWANZA YA KITANZANIA KUTAMBULIWA KAMA MWAJIRI KINARA NA TOP EMPLOYERS











NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB imekuwa Taasisi ya Kwanza ya Kitanzania kupata ithibati ya kuwa Mwajiri Kinara Tanzania kwa Mwaka 2025, inayotolewa na taasisi bobevu na mahiri ya masuala ya rasilimali watu ya Top Employers Institute ya Uholanzi, ambayo kwa mwaka huu imetoa vyeti vya uKinara kwa taasisi bora katika nchi 124 duniani.

Hii sio mara ya kwanza NMB kutambulika kama Mwajiri Kinara, kwani tayari imetunukiwa Tuzo ya Mwajiri Bora Tanzania kwa Mwaka 2023 na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), lakini pia ilipata Tuzo ya Mwajiri Bora Afrika Mwaka 2022 kutoka Employer Branding Institute, taasisi bobevu ya masuala ya ajira duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Alhamisi ya Januari 16, Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay, alisema ni fahari kwa taasisi yake kuwa miongoni mwa mashirika 2,400 duniani yaliyotambuliwa na kutunukiwa uthibitisho huo wa uKinara kwa mwaka 2025.

Alibainisha kuwa, Top Employers Institute ni taasisi kinara duniani katika kufanya tafiti na ukaguzi huru wa mashirika kuhusu rasilimali watu, ikitumia vigezo vya kimataifa na wanajivunia tuzo hiyo ambayo inathibitisha kuwa NMB ni taasisi imara ya ajira na kiongozi katika maendeleo ya rasilimali watu nchini.

"Tuzo hii kutoka Top Employers Institute ni muhimu sana kwetu kama mwajiri wa takribani watu 4,000, kwani wafanyakazi walio tayari kujitolea na wenye motisha wa kuhudumia, ni msingi wa huduma Kinara na mojawapo ya njia kuu za kuwaridhisha wateja wetu.

“Uthibitisho wa Mwajiri Kinara unathibitisha thamani ya juhudi zetu na kuimarisha shauku yetu ya kuhakikisha kila mtu anafanikiwa.

“Pia, hii tuzo inayoakisi ahadi yetu ya mazingira Kinara kazini, yenye ustawi kwa wafanyakazi, ambao wanajivunia na kufurahia ajira zao. Kama sehemu ya mkakati wetu wa biashara, tunafanya uwekezaji mkubwa wa kuwa na utamaduni jumuishi ambapo watu wetu wanahisi kuthaminiwa na kushirikishwa," alibainisha Akonaay. 

Aliongeza ya kwamba, kuna sababu kadhaa zilizowawezesha kutwaa tuzo hiyo, ikiwemo kuwa na mikakati bora juu ya wafanyakazi, upatikanaji wa wafanyakazi bora, uendelezaji wa wafanyakazi, namna bora ya kuwatumia wafanyakazi kulingana na ubora wao, utofauti na ujumuishaji na ustawi wa wafanyakazi.

Akonaay aliongeza kuwa kwa mwaka huu 2025, Taasisi ya Top Employers imetoa vyeti vya uKinara kwa taasisi mbalimbali katika nchi 124 duniani, ambazo kwa pamoja zina athari chanya kwenye maisha ya zaidi ya wafanyakazi zaidi milioni 13 kupitia mbinu Kinara za Rasilimali Watu na Mazingira Kinara ya Ajira.

“Kutunukiwa huku kwa Benki ya NMB kumetokana na kushiriki katika utafiti wa ‘Mbinu Kinara za Rasilimali Watu,’ ulioendeshwa na Top Employers Institute, kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na kuwalinganisha washiriki kwa vigezo vya mbinu Kinara za ajira zinazotambulika na kutumika duniani.

“Mchakato wa tathmini ya washiriki ulizingatia maeneo sita muhimu katika masuala ya rasilimali watu na sehemu 20 za sera na mbinu za utendaji kazi. Hizi ni pamoja na mkakati wa usimamizi na maendeleo ya wafanyakazi, upatikanaji na usimamizi wa vipaji, huduma za ustawi, utofauti na ujumuishwaji, pamoja na kuwa na mazingira rafiki ya kazi.

Alisema kwamba, tuzo hiyo inaenda kuwa chachu ya NMB kuendelea kuwa bora zaidi, huku ikiendelea kuboresha utamaduni wake katika ufanyaji kazi na kubuni mbinu bora za uajiri ili kukidhi mahitaji yanayobadilika ya wafanyakazi.

“Ulimwengu wa kazi unabadilika, na NMB tumejikita katika kukabiliana na mabadiliko haya kwa kuwekeza katika watu wetu na kukuza mazingira yanayochochea ukuaji, tutahakikisha tunabaki kwenye njia yetu ya ubora na kuifanya benki kuwa kinara katika huduma za kifedha na hata katika ustawi wa wafanyakazi wake,” alisisitiza Akonaay.

No comments:

Post a Comment