TMA YAWAPA SEMINA WANAHABARI HABARI ZA UTABIRI WA HALI YA HEWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 22 January 2025

TMA YAWAPA SEMINA WANAHABARI HABARI ZA UTABIRI WA HALI YA HEWA

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, akizungumza katika semina kwa wanahabari. 







MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa elimu kwa wanahabari wanaoandika habari za utabiri wa hali ya hewa nchini huku akiwasisitiza kuzingatia miongozo ya utoaji wa taarifa hizo kwa jamii.

Akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema wanahabari wanapaswa kutoa taarifa sahihi kwa jamii ili ziweze kuwasaidia walengwa.

“Naomba tuendelee kuielimisha jamii, huku mkitumia ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kufikisha taarifa, kufanya hivyo mnasaidia kuokoa maisha ya watu kwa kuepukana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa,” amesema Dkt. Chang’a.

Akizungumzia mabadiliko ya hali ya hewa, ameeleza kuwa mwaka 2024 kulikuwa na ongezeko la joto duniani 1.55 na kuvunja rekodi, huku nchini Tanzania takwimu zinaonesha kulikuwa na ongezeko la joto 0.7.

“Kila mwaka joto linaendelea kuongezeka hali ambayo inatokana na changamao ya uwepo wa hali ya mbaya ya hali ya hewa ikiwemo uwepo wa vimbunga” amesema Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang’a ameishukuru Serikai ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya hali ya hewa, kwani mwaka 2024 walifanikiwa kununua rada mbili ambazo zimefungwa Mkoa wa Kigoma na Mbeya na kuifanya Tanzania kuwa Nchi pekee Afrika ya Mashariki katika kuwa na vifaa bora vya hali ya hewa.

Awali akizungumza katika semina hiyo, Meneja wa Ofisi Kuu ya Utabiri TMA Dkt. Mafuru Kantamla, amesisitiza umuhimu kwa wanahabari kufanya kazi kwa kuzingatia uweledi, maadili pamoja na kuendelea kuwa na nidhamu katika kuhabarisha jamii kuhusu taarifa za hali ya hewa.

No comments:

Post a Comment