Na Asia Singano, Arusha
SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha, imeahidi kuendelea kutekeleza azma yake ya kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi wote ili kuhakikisha kuwa wanaelimika kuhusu masuala ya fedha, mikopo, uwekezaji ili kuwawezesha wananchi kutumia huduma sahihi za fedha.
Akizungumza jijini Arusha, Afisa Mwandamizi, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, wakati akitoa elimu ya fedha kwa wajasiliamali na wananchi wa Mtaa wa Muriet jijini Arusha, alisema Wizara iliona umuhimu wa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wote ili kuwajengea nidhamu ya matumizi ya fedha.
Bw. Kimaro alisema kuwa wananchi wengi wanashindwa kupiga hatua kiuchumi kutokana na uelewa mdogo juu ya matumizi sahihi ya fedha, kukosa usimamizi mzuri wa fedha zao pamoja na kutokuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba na kuwekeza hali inayosababisha baadhi ya wananchi fedha wanazopata kutobadilisha maisha yao kiuchumi.
“Imekuwa ni kawaida kusikia vilio vya wananchi wakiwa wamepata changamoto za mikopo wanakopa kwa watu wasio rasmi kutokana na kukosa uelewa wa wapi wanapaswa kukopa na namna ya kutumia hiyo mikopo jambo linalowaletea madhara” alisema Bw. Kimaro
Akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya uwekezaji, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoani Arusha, Bw. Josephat Komba, aliwataka wajasiriamali kuwekeza sehemu sahihi ili kuepuka kupoteza fedha zao.
‘’Nawasihi kuwekeza kwenye maeneo ambayo fedha zenu zitakuwa salama na mtapata faida, karibuni kuwekeza NSSSF, kwakuwa kwa kila kiasi cha fedha zako unachoweka utapata akiba na utapata bima ya afya’’ alisema Bw. Komba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Muriet, Bw. Rashid Juma, aliwataka watoa huduma za fedha katika mtaa huo kufuata sheria na taratibu za huduma ndogo za fedha kama mafunzo yalivyotolewa na timu ya wataalam wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha.
‘’Natoa onyo kwa watoa mikopo mtaani kwangu, ni marufuku kumfuata mtu usiku wa manane kudai pesa, wengine wanaingia kwenye matatizo wanaitiwa wezi wanapigwa kumbe sio wezi wameenda kudai mikopo, kopesheni kwa kufuata taratibu zilizowekwa’’ alisema Bw. Juma.
Hii ni Awamu ya Tatu ya Elimu ya Fedha inayotolewa na Wizara ya Fedha, ambapo kwa awamu hii mikoa mbalimbali inatarajiwa kufikiwa ikiwemo mkoa wa Arusha ambapo imeanza kutolewa huku mikoa mingine ikiwa ni Kilimanjaro, Mwanza pamoja na Mkoa wa Mara lengo likiwa ni kuwapa elimu wananchi kuhusu masuala ya fedha ikiwemo matumizi sahihi ya fedha binafsi, uwekaji akiba uwekezaji.
No comments:
Post a Comment