Na Mwandishi Wetu, Unguja
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad
Yussuf Masauni amesema msimu ujao wa Ligi ya Muungano utaboreshwa zaidi ikiwa
pamoja na zawadi kwa bingwa ili kuipa hadhi ya kipekee ligi hiyo.
Amesema lengo ni kuifanya ligi hiyo inakuwa moja ya ligi bora
Afrika Mashariki na kuifanya kuwa na mvuto wa aina yake kwa wapenda soka
akieleza kuwa michezo ndio sehemu ambayo jamii hukutana na kuongea lugha moja.
Mhe. Masauni ameyasema hayo Mei, 24, 2026 Unguja, Zanzibar
wakati wa halfa ya utoaji
tuzo na zawadi kwa walioshiriki na kufanikisha Ligi ya Muungano 2026 ambapo
Simba ilitawazwa mabingwa kwa kuifunga Yanga bao 1-0 katika mchezo uliochezwa
Uwanja wa Amaan Complex.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar zimeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha Muungano
kwa misingi ya Kikatiba, Kihistoria, Mshikamano wa Kitaifa na maendeleo ya
pamoja.
“Juhudi hizo zinajielekeza kuhakikisha kuwa jamii ya Watanzania
inakuwa na umoja na ushirikiano katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na
kisiasa.
Mhe. Masauni amesema, Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ndiyo yenye
dhamana na masuala ya Muungano kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imeamua kuwa sehemu ya uratibu wa Ligi ya Muungano ili kuongeza nguvu.
Amesema hatua hii itasaidia kuboresha maandalizi ya ligi ikiwemo
kuboresha zawadi kwa washiriki na mshindi wa ligi.
“Nizipongeze timu zote ambazo zilishiriki mashindano haya kwa
mwaka 2026 maana ushiriki wao ndio mafanikio ya uwepo wa Ligi hii ya Muungano.”
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo
Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma amesema pamoja na ligi hiyo kusimama kwa muda
mrefu lakini ilipotangazwa kurejea wadau waliitikia vizuri na kutoa
ushirikiano.
“Awali kama wizara tulianza kwa wasiwasi lakini mwisho tulimaliza
kwa furaha kwani tumegundua michezo imekuwa kitu cha kipekee na tutazidi
kushirikiana na kumalizika kwa msimu huu inafanya tuanze maandalizi kwa ajili
ya mwaka ujao,” amesema Mhe. Dkt. Riziki.
Naye, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar
(ZFF), Hussein Ahmada amezishukuru serikali za pande zote mbili kwa
kuifanya michezo kuwa moja ya eneo la kuwaunganisha Watanzania kupitia Ligi ya
Muungano akieleza kuwa hali hiyo imekuwa faraja kwa wapenda soka kuona nao
wanathaminiwa.
Mwaka huu ligi hiyo
ilishirikisha timu nane ambazo ni Simba iliyotwaa ubingwa, Yanga, Azam na
Singida Black Stars kutoka Tanzania Bara wakati kwa Zanzibar ilikuwa Mlandege,
KVZ, Mafunzo na Muembe Makumbi.
.jpg)
.jpg)

No comments:
Post a Comment