SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limebainisha kuwa, limejipanga kuendana na kauli mbiu ya Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya ‘Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji’ kwa kile kufungua milango ya kidigitali kwa wawekezaji na Wafanyabiashara ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi Zaidi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL, Bi. Zuhura Muro alipotembelea Banda la Maonesho la Shirika hilo kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Temeke Jijini Dar es Salaam.
Bi. Zuhura amesema shirika linao wajibu mkubwa wa kuunganisha mawasiliano nchini na hata nje ya mipaka ya nchi, lengo likiwa ni kurahisisha biashara na kufanya utekelezaji wa majukumu kwa wawekezaji kuwa rahisi na ubora unaotakiwa.
Amesema TTCL kwa muda sasa imekuwa ikifungua milango ya kidigitali na nchi karibu zote zinazopakana na Tanzania kwa kuunganisha nchi hizo kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasliano, hivyo bado shirika linalo jukumu la kuunganisha dunia kidigitali kutokana na ubora wa mawasiliano yanayotolewa na shirika hilo.
"Sisi kama TTCL tunafungua milango ya kidigitali na nchi zinazotuzunguka hivyo tunao mkakati wa kuunganisha Tanzania na Dunia kidigitali kutokana na ubora wa Mawasiliano tulionao," amesema Muro.
Amesema pia TTCL ipo tayari kufanya ushirikiano na wawekezaji kwa lengo la kupata huduma nzuri ya Mawasiliano na hivyo kuzikaribisha Taasisi, Makampuni na Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara na shirika hilo kutokana na ukweli kuwa huduma zinazotolewa ni za uhakika na salama.
“Tunazikaribisha Kampuni na Wafanyabiashara kushirikiana nasi kwani tunaamini ushirikiano huo utawawezesha wawekezaji kufanya shughuli zao mbalimbali ikiwemo ya kibiashara kwa kutumia Mawasiliano yetu,"amesema.
Amesema TTCL imekuwa ikiendesha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hivyo Shirika limejipanga kuendesha biashara kila sehemu ikiwemo maeneo ya utalii ili kuunga mkono juhudi za kukuza sekta ya utalii nchini kwa kuweka mawasiliano ya Intaneti ili kuyaongezea thamani maeneo hayo ya kitalii.
No comments:
Post a Comment