Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI Mkoa wa Singida chini ya Mkuu wa Mkoa huo Dk.Binilith Mahenge leo asubuhi wamemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka baada ya kumaliza mbio zake mkoani humo.
Akisoma hotuba ya makabidhiano Dk. Mahenge alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Singida ulikibimbizwa umbali wa Kilometa 642.3 na jumla ya miradi 55 yenye gharama ya zaidi ya Sh. 8 Bilioni iliwekewa mawe ya msingi, kuzinduliwa, kufunguliwa na kutembelewa katika sekta za maji, Elimu, Afya, Utawala Bora, Barabara, uwezeshwaji wa Wananchi Kiuchumi na program za mapambano ya UKIMWI, Maralia, Rushwa , mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya, Umuhimu wa Lishe na Matumizi sahihi ya Tehema, ambapo miradi yote ilikubaliwa na Mwenge huo wa Uhuru.
Mahenge aliwapongeza Vijana Sita Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakiongozwa na Luteni Josephine Mwambashi na wenzake Luteni Ramadhani Msham, Luteni Geofrey Aron, Luteni Mussa Mussa ,Coplo Rehema Haji na PTE Dismas Mvula kwa kazi nzuri na kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kazi hiyo muhimu ya kukimbiza Mwenge wa Uhuru na Ukaguzi wa Miradi kwa kina.
Aidha Mwenge wa Uhuru ulitoa ujumbe kwa Wananchi unaohusiana na Tehema chini ya kauli mbiu TEHEMA ni Msingi wa Taifa endelevu; Itumie kwa usahihi na Uwajibikaji pamoja na mapambano dhidi ya UKIMWI ,Maralia, Rushwa , Mapambano dhidi Dawa za Kulevya na umuhimu wa Lishe Bora na vijana sita walifafanua ujumbe wote.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa LT Josephine Mwambashi akiwaaga wananchi wa Mkoa wa Singida wamempongeza Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Singida Frederick Ndahani na Timu yake kwa Uratibu mzuri wa mbio za Mwenge na kuwa ulikuwa mzuri na umesaidia kufanikisha mbio hizo mkoani humo.
Pia Mwambashi amewapongeza Wakuu wa Wilaya zote kwa usimamizi wa miradi uliosababisha miradi yote kukubaliwa.
Mratibu wa Mwenge wa uhuru Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani ambaye pia ni Afisa Vijana wa Mkoa, amewashukuru wananchi, viongozi wa Serikali na Taasisi , Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa wakiongozwa na Chama Tawala CCM , Wakurugenzi, Makatibu Tawala, Timu ya Uratibu Mkoa,Waratibu wa Mwenge Wilaya na Wakuu wa Wilaya kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika Mbio za Mwenge wa uhuru mkoani Singida.
No comments:
Post a Comment