Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe mkoani Tanga, Ntuli Danken, akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea banda la TEA kwenye Maonesho ya Wiki ya Taifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026, yanayofanyika katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga Agosti 17, 2026.
Na Mwandishi
Wetu, Tanga
WANAFUNZI wa
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe mkoani Tanga, wameishukuru Wizara ya
Elimu kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kuwapatia vifaa vya mafunzo ya Amali.
Pongezi hizo
wamezitoa wakati wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea banda la
TEA kwenye Maonesho ya Wiki ya Taifa ya Elimu, Ujuzi na
Ubunifu 2026, yanayofanyika katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga Agosti 17,
2026.
“ Tunaishukuru
Serikali kwa kutupatia mafunzo ya Amali na vifaa vya kujifunzia kwa mfano mimi
nasomea mapishi ya aina mbalimbali naamini nikirudi nyumbani nitafanya shughuli
zangu kitaalamu,” alisema Ntuli Danken mwanafunzi wa kidato cha tatu katika
shule hiyo.
Alisema
mafunzo ya Amali yana fursa nyingi kwani mwanafunzi akimaliza masomo yake ya
kidato cha nne anaweza kujiajiri au kuajiriwa na hata anapokuwa akisubiri
matokeo yake ataweza kujiingizia kipato.
Ntuli alisema
changamoto iliyopo kwa baadhi ya wazazi ni kuwakataza watoto wao wasisome Amali
kwa madai kuwa haina faida yoyote jambo ambalo siyo la kweli.
“Mwanafunzi
akifeli iwapo atakuwa amejifunza Amali itamsaidia kufanya shughuli zake na
kupata fedha za kumsaidia katika maisha yake ya kila siku,” alisema Ntuli.
Mwanafunzi
mwingine wa shule hiyo, Najma Baraka wa kidato cha tatu ambaye naye anasoma
Amali aliishukuru Serikali na TEA kwa kuwapelekea vifaa vya kujifunzia masomo
ya Amali.
“Zamani kabla ya kuletewa vifaa tulikuwa
tunajifunza bila ya vitendo lakini sasa tunaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali
kutokana na vifaa tulivyo letewa,” alisema Najma.
Alisema
masomo ya Amali yanawasaidia sana na atakapo maliza masomo yake ya kidato cha
nne atakuwa na vyeti viwili cha NECTA na Amali ambapo kabla matokea hayajatoka
atakuwa akitengeneza na kuuza bidhaa zake mbalimbali.
Mwalimu
Catherine Machugu wa shule hiyo ambaye anafundisha masuala ya mapishi wanafunzi
wa kidato cha tatu ameishukuru Serikali kupitia TEA kwa kuwafadhili vifaa
mbalimbali ambavyo vinawasaidia wanafunzi walio mkondo wa Amali kusoma kwa
ufanisi na uelewa zaidi.
Alisema shule hiyo ina jumla ya Amali 5 na ilipokea vifaa vyenye thamani ya zaidi ya milioni 400 kwa ajili ya Amali hizo ili kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji
“Vifaa hivi vimesaidia kuongezeka kwa usajili wa wanafunzi tofauti na hapo awali,” alisema Mwalimu Machugu.




No comments:
Post a Comment