Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Peter Msoffe, akimkabidhi Tuzo ya Heshima mke wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk.Geoffrey Mkamilo, Prisca Mkamilo kwa kutambua mchango katika Maadhimisho ya miaka 10 tangu ianzishwe taasisi hiyo katika hafla iliyofanyika Agosti 3, 2026. Katikati ni Joshua Mkamilo.
Na Dotto Mwaibale, Dodoma
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake kwa kumuenzi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wake wa kwanza, Dk. Geoffrey Mkamilo, kwa kumtunuku tuzo ya heshima kutokana na mchango wake mkubwa katika kuasisi na kujenga taasisi hiyo hadi kufikia mafanikio ya sasa.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Agosti 3, 2026, kwenye Viwanja vya Nane Nane Nzuguni jijini Dodoma, TARI ilieleza kuwa Dk. Mkamilo aliiongoza taasisi hiyo katika kipindi kigumu cha mwanzo, ambapo haikuwa na ofisi wala fedha za kuendesha shughuli zake.
Licha ya changamoto hizo, alisimamia kwa uthabiti ujenzi wa msingi imara wa taasisi, akisaidiana kwa karibu na aliyekuwa Katibu Muhtasi wake, Mary Lema, ambaye pia alitunukiwa tuzo ya heshima kwa mchango wake.
Mbali na Dk. Mkamilo na Mary Lema, tuzo nyingine zilitolewa kwa watafiti na watumishi mbalimbali waliochangia maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia ubunifu na tafiti zenye tija.
Miongoni mwa waliotunukiwa ni Dk. Evarine Lukonge, Dk. Malela na Elizabeth Mziray, pamoja na wataalamu waliofanikisha maboresho katika mazao mbalimbali ikiwemo pamba, muhogo na korosho, huku baadhi wakitambuliwa kwa kubuni teknolojia na mashine zilizoongeza tija katika uzalishaji wa kilimo nchini.
TARI pia iliwatunuku tuzo wadau wake mbalimbali kwa kutambua ushirikiano na mchango wao katika kuimarisha tafiti za kilimo na kuendeleza ubunifu unaochochea maendeleo ya sekta hiyo.
Tuzo ya marehemu Dk. Geoffrey Mkamilo, aliyefariki dunia Machi 2, 2024, jijini Dodoma, ilipokelewa na mke wake, Prisca Mkamilo, pamoja na Joshua Mkamilo, katika hafla iliyogubikwa na hisia za heshima na shukrani kwa mchango wake wa kizalendo.
Akihitimisha maadhimisho hayo baada ya kukabidhi tuzo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Peter Msoffe, alisema Serikali ina imani kubwa na TARI katika kutoa tafiti na ushahidi wa kisayansi unaosaidia kufanya maamuzi sahihi kwa maendeleo ya sekta ya kilimo.
Alisisitiza kuwa taasisi hiyo inapaswa kuendelea kuongoza katika kuboresha uzalishaji wa mazao, kuimarisha mifumo ya masoko, kuendeleza teknolojia za kilimo, pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha kilimo kinaendelea kuwa nguzo ya uchumi na usalama wa chakula npchini.Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Peter Msoffe, akimkabidhi Tuzo ya Heshima, Mary Lema aliyekuwa Katibu Muhtasi wa Dk. Geoffrey Mkamilo.
Hafla hiyo ikiendelea.
Mary Lema (kulia) aliyekuwa Katibu Muhtasi wa Dk. Kamilo na Mke wa Dk.Kamilo Prisca Mkamilo wakionesha Tuzo.

No comments:
Post a Comment