MKAPA ALIKUWA MKWELI KWA NYERERE, ALIKIRI ALIJUA KUANDIKA, LAKINI HAKUJUA KUSIMAMIA GAZETI... - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 25 July 2020

MKAPA ALIKUWA MKWELI KWA NYERERE, ALIKIRI ALIJUA KUANDIKA, LAKINI HAKUJUA KUSIMAMIA GAZETI...

Ben Mkapa
Kwenye Uhai Wake:

Mkapa Alikuwa Mkweli Kwa Nyerere, Alikiri Alijua Kuandika, Lakini Hakujua Kusimamia Gazeti...

- Ni pale Nyerere alipomwomba Mkapa awe Mhariri Mkuu wa gazeti la Chama.

Ndugu zangu,

Ben Mkapa kwenye kitabu chake; My Life, My Purpose, anaeleza alivyoshtuka siku ile Nyerere alipomwambia awe Mhariri wa gazeti la Chama la Kiingereza ‘ The Nationalist’.

Nyerere hakufurahishwa jinsi gazeti hilo lilivyoendeshwa.

“ Ben, I think you can help us, I want you to be the editor of ‘ The Nationalist’, I think you can do it, can you?”

I nervously replied, “ Mr President I know I can write, but this is a newspaper, I know next to nothing.” ( Benjamin Mkapa, My Life, My Purpose- Tanzanian President remembers, pg. 53)

Mkapa alikuwa mkweli kwa Nyerere. Ni kwa kusema aliweza kuandika, lakini hakuwa na alilolijua kuhusu shughuli za kusimamia gazeti.

Ilikuwa ni Nyerere na  Katibu wake Myeka, mwanamama Mwingereza, Joan Wicken waliomwunganisha  Mkapa na gazeti la ‘ The Mirror’ la Uingereza ambapo Nyerere alimjua mmoja wa viongozi wa gazeti hilo na Joan Wicken alimjua mke wa kiongozi huyo wa gazeti la The Mirror.

Hivyo, Mkapa akaambiwa atapangiwa taratibu za kwenda huko Uingereza akajifunze mambo ya magazeti kwa miezi kadhaa na akirudi nyumbani Nyerere angemteua kuwa mhariri.

Ikaja kuwa hivyo, Mkapa akawa Mhariri wa ‘ The Nationalist’. Nyerere , mbali ya kuwa Rais wa Jamhuri, alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti hilo na Joan Wicken akibaki kuwa Katibu Myeka wa Nyerere.

Ni Joan Wicken aliyepanga ratiba za Nyerere na hata kumwandikia hotuba. Joan Wicken alikuwa msomi wa Falsafa, Uchumi na Siasa.

Mwanamama huyu Mwingereza Joan Wicken , alifanya kazi kwa karibu pia na Ben Mkapa, na ameandika mengi kwenye shajara zake. Ni kwa miaka 30 akiwa Katibu Myeka wa Mwalimu.

Ameandika mengi ya kujaza maboksi kwa masanduku kuhusu waliyokuwa wakiyazungumza na Nyerere.

Hata siku alipoamua kuondoka Tanzania, hakuthubutu kuyaacha maandiko yake binafsi kwenye shajara yake akihofia watendaji wa hapa nchini wasingezingatia maagizo ya wosia wake.

Kwenye wosia wake ametaka akifa shajara hizo zifungiwe hadi ifike miaka 30 baada ya kifo chake ndipo zifunguliwe kwa yeyote kusoma. Ni maandiko yenye siri kubwa pia juu ya taifa letu, na pia juu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Joan Wicken alikufa mwaka 2004. Hivyo, ni mwaka 2034 ndipo zitasomwa.

Kwenye kitabu chake, Mkapa alimwelezea mama huyo. Akaelezea pia hisia na matamanio yake ya kuyasoma yaliyoandikwa na Joan Wicken. Lakini, Ben Mkapa, labda kwa kuanza kuziona ishara za umauti uliokuwa njiani pia, aliandika kwa kalamu yake, kuwa hakutajia kuishi kuyasoma ya Joan Wicken.

Ben  Mkapa angeishi mpaka kufikisha miaka 96, basi, naye angeyasoma yaliyoandikwa na mwenzake kwenye utumishi enzi za Mwalimu.

Apumzike Kwa Amani.

Maggid Mjengwa.
Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment