RADA ZA HALI YA HEWA NI MUHIMU KATIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 28 January 2026

RADA ZA HALI YA HEWA NI MUHIMU KATIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NCHINI





MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) iliandaa warsha ya mafunzo ya Rada za Hali ya Hewa na matumizi ya taarifa zinazotokana na Rada,  tarehe 26-27 Januari 2026, Dodoma. Lengo kuu la mafunzo haya ni kuimarisha uwezo wa kitaalamu na kiufundi katika matumizi ya teknolojia Rada, hususan katika uchambuzi, tafsiri na matumizi ya taarifa ili kuboresha utoaji wa utabiri zikiwemo tahadhari za  hali mbaya ya hewa kwa wakati na kwa usahihi zaidi.    

Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa warsha hiyo alikuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema “Kama mnavyofahamu, kwa sasa dunia inashuhudia ongezeko kubwa la matukio ya hali mbaya ya hewa yanayotokana na  kuchagizwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, ikiwemo mvua kubwa, mafuriko, vipindi virefu vya ukame, pamoja na matukio ya vimbunga na upepo mkali.  Matukio haya yamekuwa  ya mara kwa mara na ya hatari zaidi. 

Katika kipindi hiki huduma za tahadhari dhidi ya hali mbaya ya hewa ni muhimu sana hususani kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, kwani uchumi wetu unategemea sana sekta za kijamii na kiuchumi zinazotegemea hali ya hewa. Katika muktadha huu uimarishaji wa miundombinu ya utoaji wa huduma za hali ya hewa ikiwemo uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali  wa kuimarisha mifumo ya Rada za hali ya hewa ni hatua kubwa na muhimu sana katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Aidha, Mratibu  wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mradi wa Kuboresha Mfumo wa Utoaji wa Tahadhari za Hali Mbaya ya Hewa “Climate Risk and Early Warning Systems (CREWS) kwa ufadhili wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)” Bi. Mecklina Merchades  alisema mafunzo hayo yanalenga katika kuhakikisha wataalam wanakuwa na ujuzi wa kutosha katika kutumia mifumo ya Rada kama nyenzo muhimu ya kuboresha ufuatiliaji na utabiri wa matukio ya hali mbaya ya hewa, yenye athari kwenye sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. 

TMA inaendelea kuishukuru Serikali kwa uwekezJi mkubwa katika kuimarisha rasilimali watu, miundombinu, teknolojia na mifumo ya kisasa kwa lengo la kuboresha huduma za tahadhari na kuchangia katika kulinda maisha, mali na ustawi wa jamii.

No comments:

Post a Comment