Na Saidina Msangi na Joseph Mahumi, WF, Dodoma
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yoichi Mikami na Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Sakphouseth Meng, ambapo wamejadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo nishati na kilimo.Akiwa na Balozi wa Japan, Mhe. Balozi Omar aliishukuru nchi hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa kusaidia utaalam, mikopo nafuu na misaada ya kiufundi ambayo imeisadia Tanzania kupiga hatua kupitia sekta za kilimo, elimu, na viwanda.
Aidha, Mhe. Balozi Omar aliwaalika wawekezaji kutoka Japan kuja kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali zenye kuleta tija kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yoichi Mikami, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na nchi yake, na kwamba kuna idadi kubwa ya Wajapan, waliowekeza na kutaka kuja kuwekeza nchini Tanzania na kuiomba Serikali iendelee kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Katika Tukio lingine, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Omar, aliushukuru Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo IFAD kwa kuwekeza dola za Marekani bilioni 2 tangu uanze kushirikiana na Tanzania katika kukuza kilimo, nishati na miradi mingine ya kijamii.
Alimweleza Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko Huo nchini Tanzania Mhe. Sakphouseth Meng, kwamba Tanzania inaukaribisha mpango mpya wa 14 wa Mfuko huo utakaotekelezwa nchini ambapo Mfuko huo unatarajia kuwekeza kati ya dola za Marekani milioni 60 hadi milioni 70 kwenye maeneo ya kilimo, nishati, miundombinu katika maeneo ya vijijini.
‘‘Tanzania inafurahia ushirikiano kati yake na IFAD ambao umeanza muda mrefu tangu mwaka 1978 na tumekubaliana kuimarisha ushirikiano huu, kwa kuangalia zaidi maeneo yanayohitaji rasilimali kwa kutumia taasisi za fedha za ndani ikiwemo Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo TADB ambayo imekuwa ikifanya vizuri’’, alisema Mhe. Balozi Omar.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo-IFAD, nchini Tanzania, Bw. Sakphouseth Meng, aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuendeelea kusimamia vizuri uchumi wa nchi na kwamba IFAD itaendelea kuwekeza zaidi katika sekta za kiuchumi na kijamii kupitia mpango wake wa kuwainua wananchi masikini wanaoishi maeneo ya vijijini.
.jpg)

No comments:
Post a Comment