RAIS DKT. SAMIA AHUTUBIA UZINDUZI JUKWAA LA UWEKEZAJI BARANI AFRIKA (GAIS), UAE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 4 February 2026

RAIS DKT. SAMIA AHUTUBIA UZINDUZI JUKWAA LA UWEKEZAJI BARANI AFRIKA (GAIS), UAE

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia katika uzinduzi wa Jukwaa la Uwekezaji barani Afrika (GAIS), Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu tarehe 03 Februari, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Rais wa Angola ambaye pia Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Mhe. João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Ghana Mhe. John Mahama wa pili kutoka (kushoto), Waziri Mkuu wa Msumbiji Mhe. Maria Benvinda Levy wa kwanza (kushoto), Mwanzilishi Mwenza na Mwenyekiti Mtendaji wa GAIS na Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina pamoja na Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa APCO Worldwide, Bi. Margery Kraus wa kwanza (kulia) mara baada ya uzinduzi rasmi wa Jukwaa la Uwekezaji barani Afrika (GAIS), uliofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu tarehe 03 Februari, 2026.

TANZANIA YATHIBITISHA DHAMIRA YAKE KUIMARISHA UAMINIFU,

MIUNDO THABITI NA UTEKELEZAJI CHINI YA

GLOBAL AFRICA INVESTMENT SUMMIT

UZINDUZI rasmi wa Global Africa Investment Summit (GAIS), unaashiria mabadiliko ya

kimkakati jinsi Afrika inavyoshirikiana kupata mitaji ya kimataifa kwa kuzingatia

uwekezaji uliopangwa kwa viwango vya kitaasisi, unaoendana na vipaumbele vya kitaifa

na faida za muda mrefu.

Uzinduzi huo, uliofanyika ulifanyika jana, Jumanne usiku, kando ya World Governments

Summit jijini Dubai, uliwakutanisha baadhi ya Wakuu wa Nchi za Afrika, watunga sera,

wawekezaji wa kimataifa na viongozi wa biashara, kutambua kwamba changamoto ya

ukuaji wa Afrika si ukosefu wa rasilimali, bali ni miundo, na kwamba pengo hilo sasa

linashughulikiwa kwa kimkakati zaidi.

Katika hotuba yake, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya

Muungano wa Tanzania, alithibitisha utayari wa Tanzania kushiriki GAIS kama mshirika

wa kuaminika na wa muda mrefu katika uwekezaji.

“Kile wawekezaji wanachotafuta leo si fursa pekee, bali ni uaminifu - uaminifu kwa taasisi,

uthabiti wa sera, na serikali zinazotekeleza ahadi zake.”

Rais Samia alitolea mfano uwekezaji wa makusudi wa Tanzania katika miundombinu ya

msingi, yaani nishati, usafirishaji na uchukuzi - ili kuchochea uzalishaji, viwanda na

ujumuishaji wa kikanda.

2/3

Miradi mikubwa katika umeme wa maji, reli ya kisasa, bandari na barabara, sambamba

na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs) na Kituo cha Huduma za Uwekezaji cha Dirisha

Moja, (TISEZA), imepunguza vikwazo kwa wawekezaji na kuimarisha imani yao kwa

Tanzania.

Aliongeza kuwa majukwaa kama GAIS yanaiwezesha Afrika, hususan Tanzania,

kuhama kutoka utamaduni wa kutangaza miradi isiyoungana na kuhamia katika

ushirikiano unaoendana na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa, na matarajio ya

wawekezaji.

Zaidi ya Mkutano, GAIS imejipambanua kama mwezeshaji wa miundombinu ya soko,

mwenye lengo la kubadilisha mali za umma na za kitaifa za Afrika kuwa maeneo ya

uwekezaji yaliyoandaliwa vyema, yasiyo na madhara kubwa kibiashara, yanayokidhi

viwango vya kimataifa vya utawala, na usimamizi wa athari zinazoweza kuathiri faida.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Dkt. Akinwumi Adesina, Mwanzilishi Mwenza na

Mwenyekiti Mtendaji wa GAIS pamoja na Rais wa zamani wa Benki ya Maendeleo ya

Afrika, alisema: “Tatizo si ukosefu wa rasilimali, bali ni ukosefu wa miundo ya

kuaminika inayounganisha rasilimali hizo na mitaji ya kimataifa.”

Alibainisha kuwa rasilimali za kimkakati za Afrika katika nishati, madini, miundombinu

na mtaji wa asili bado hazijathaminiwa ipasavyo kutokana na miundo dhaifu, taarifa

zisizo kamilifu, mifumo ya utawala iliyogawanyika na gharama kubwa za tathmini ya

uwekezaji (due diligence).

GAIS inalenga kushughulikia vikwazo hivyo kwa kuongeza uwezo wa kukuza miradi,

kutabirika na kuwa na ushirikiano wa muda mrefu.

“Afrika lazima ihame kutoka utegemezi wa misaada kwenda ukuaji unaoongozwa na

uwekezaji,” alisisitiza.

Mheshimiwa João Lourenço, Rais wa Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika,

alisema GAIS inaakisi ukomavu wa kisiasa wa Afrika na utayari wake wa kushirikiana

na mitaji ya kimataifa kwa uwajibikaji na ushindani.

“Afrika lazima ichukue umiliki mkubwa wa mali zake za kitaifa na kuzitumia kwa njia

zinazoharakisha maendeleo,” alisema Rais Lourenço.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa sheria zinazotabirika, mikataba yenye uwazi, na uthabiti

wa sera, akitaja mageuzi ya Angola, ikiwemo ubinafsishaji, dirisha moja la uwekezaji, na

miradi ya mpito wa nishati, kama ushahidi wa dhamira ya mageuzi na utekelezaji.

Wakati huohuo, Mheshimiwa John Mahama, Rais wa Jamhuri ya Ghana, alisisitiza haja

ya Afrika kubadili namna mitaji ya kimataifa inavyoshirikiana na bara hili, akisema:

“Afrika haina upungufu wa rasilimali. Kinachohitajika ni usanifu unaoruhusu mali hizo

kuzungumza lugha ya mitaji ya kimataifa.”

3/3

Alitaja mageuzi ya sekta ya dhahabu na madini nchini Ghana, ikiwemo kudhibiti

usafirishaji wa madini ghafi, kama mifano ya jinsi uundaji upya wa mali na uongezaji

thamani vinavyoweza kufungua mapato, ajira na viwanda, na kuongeza kuwa GAIS

itatoa usanifu unaoeleweka na mitaji ya kimataifa, sambamba na udhibiti wa vihatarishi

vya utekelezaji.

Kwa Tanzania, GAIS inatarajiwa kutoa fursa ya kimkakati ya kuvutia mitaji binafsi na ya

taasisi katika sekta za kipaumbele, kupunguza shinikizo kwa fedha za umma kupitia

ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP), ubia wa kibiashara (joint ventures), Vyombo

Maalum vya Utekelezaji (SPVs) na fedha mchanganyiko (blended finance), sambamba na

kuharakisha viwanda, kuongeza mauzo ya nje na kutengeneza ajira kwa vijana.

Hivyo, Tanzania itaweka mkazo katika maeneo matatu yanayohusiana:

1. Bandari, uchukuzi na biashara ya Kikanda kwa kutumia ukanda wake wa pwani

na mtandao wa bandari kama lango la Afrika Mashariki na Kati;

2. Nishati na Maeneo ya Viwanda, kwa kuimarisha uzalishaji, uongezaji thamani na

usalama wa nishati; na

3. Nafasi ya kuwa mhimili ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa

kuiweka Tanzania kuwa kitovu cha kikanda cha uzalishaji, usafirishaji na

uchukuzi na uwepo wa nishati ya kutosha na ya Uhakika.

Kwa mtazamo wa kutoka utegemezi wa misaada kwenda katika ukuaji unaoongozwa na

uwekezaji, GAIS inafungua njia za ajira kwa vijana, uhamishaji wa ujuzi, ukuaji wa

biashara za ndani, pamoja na kukuza ushiriki wa mitaji binafsi.

TAARIFA KWA MHARIRI

Global Africa Investment Summit (GAIS) ni jukwaa la uwekezaji la bara la Afrika

lililoanzishwa kwa pamoja na Dkt. Akinwumi Adesina, Rais wa zamani wa Benki ya

Maendeleo ya Afrika, na Bi. Margery Kraus, Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa

APCO Worldwide.

Mkutano wa kwanza wa Global Africa Investment Summit unatarajiwa kufanyika

baadaye mwaka 2026.

Bakari S. Machumu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.


No comments:

Post a Comment