HOTUBA YA DKT. SAMIA, KWA AJILI YA KUUAGA MWAKA 2025 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2026 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 1 January 2026

HOTUBA YA DKT. SAMIA, KWA AJILI YA KUUAGA MWAKA 2025 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2026

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA AJILI YA KUUAGA MWAKA 2025 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2026, TAREHE 31 DESEMBA, 2025 – TUNGUU, ZANZIBAR. 

Ndugu Wananchi na Watanzania wenzangu; Hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Neema na Rehema, kwa kutufikisha salama mwishoni mwa Mwaka 2025, na Inshallah, kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, tutaweza kuuona na kuuvuka pia salama Mwaka 2026. Katika mwaka huu tunaoumalizia, tumeondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zetu, ambao wametangulia mbele ya haki. 

Tuendelee kuwaombea rehema za Mwenyezi Mungu ili roho zao zipumzike kwa amani! Aidha, kwa Watanzania wenzetu ambao wanaupokea mwaka mpya wakiwa na changamoto za kiafya na shida mbalimbali, tuelekeze dua na sala zetu kwa Mwenyezi Mungu, tuombe tahafifu ili tujaaliwe wepesi wa shida zote. 

 Ndugu Wananchi; Mtakubaliana nami kwamba, katika mwaka 2025, nchi yetu iliendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika sekta mbalimbali na katika kuboresha maisha ya wananchi. Shughuli za kimaendeleo zilizofanyika katika maeneo yenu mnazifahamu vizuri, tulieleza kwa kina katika nyakati za matukio mbalimbali. Hivyo, sina haja ya kuzirejea tena hapa leo.

 Kwa ujumla, Serikali yetu imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uchumi wa Taifa, ikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei hasa za chakula. Kwa mwaka huu wa 2025, wastani wa mfumuko wa bei 2 nchini ni asilimia 3.4. Aidha, Pato la Taifa limeendelea kukua kufikia asilimia 5.8 ikilinganishwa na asilimia 5.2 ya mwaka uliopita 2024. Vilevile, Deni la Taifa linaendelea kuwa himilivu. Serikali inaendelea na mipango ya kulipa kwa haraka mikopo ya zamani yenye riba kubwa, na kurefusha muda wa kulipa mikopo, hatua itakayosaidia kupunguza kiasi cha riba iliyokuwa ikilipwa, na kutoa ahueni kwa Serikali katika kulipa mikopo hiyo. 

Ukuaji wa uchumi nchini umetokana na uwekezaji wa Serikali katika miradi ya kimkakati ya miundombinu, pamoja na mchango mkubwa wa sekta za madini, kilimo, ujenzi, na sekta ya fedha na huduma, ikiwemo Utalii. Aidha, akiba za fedha za kigeni imeendelea kuimarika na kufikia dola za Marekani bilioni 6.6, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi mitano. Tunaingia mwaka 2026, na tunaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Mwaka 2050, ambapo Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Muda wa Kati wa miaka mitatu (2025/2026 - 2027/2028), wa Kuongeza Mapato ya Serikali kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato, katika kufanya malipo, na kuongeza umakini katika usimamizi wa fedha na rasilimali za umma. 

Ndugu Wananchi; Pamoja na mafanikio hayo, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwemo utekelezaji wa ahadi za siku mia moja (100) tulizotoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu, ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Serikali itatoa taarifa kwa umma baada ya kutimia siku mia moja (100), mwezi Februari, mwakani 2026. 3 Ndugu zangu Watanzania; Katika kipindi cha miezi saba kuanzia mwezi Mei hadi Oktoba, 2025 tulikumbwa na uhaba wa mvua, hali ambayo ilileta ukame na kupungua kwa vyanzo vya maji. 

Nitumie fursa hii kuwapa pole wananchi na wakaazi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine yote ambayo kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama. Katika kukabiliana na hali hiyo, hususan kwa Dar es Salaam, Serikali ilihakikisha kwamba vyanzo vyote vya maji vilivyo karibu vinaelekeza maji Jijini humo, pamoja na kufufua visima vilivyokuwa havifanyi kazi. 

Aidha, tunamshukuru Mungu kwamba mvua zinazoendelea kunyesha ndani ya mwezi huu wa Desemba zinaongeza kina cha maji kwenye vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini, na zinarejesha hali nzuri ya upatikanaji wa maji. Katika hatua nyingine, Serikali inaendelea na ujenzi wa Bwawa la Kidunda na ujenzi wa awamu ya pili ya mradi wa maji wa Kimbiji Mpera ili tuweze kuondosha kabisa shida ya maji Mkoani Dar es Salaam na Mikoa jirani, hata katika hali ya ukame. 

Hatahivyo, katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, miezi ya Novemba na Desemba, maeneo mengine ya nchi yetu yameshuhudia mvua na upepo mkali ulioleta hasara na kubomoka kwa nyumba na kupoteza maisha. Kwa masikitiko makubwa tunatoa pole kwa wote waliofikwa na kadhia hiyo. Nazitaka Kamati za Maafa za Wilaya kuchukua hatua stahiki ili kuweza kuwasaidia wananchi hao. Aidha, ni vyema kwa Mikoa iliyopata mavuno mazuri, kuweka akiba ya chakula ili kitufae katika siku za usoni. 4

Ndugu Wananchi; Kufanya kazi kwa bidii, mshikamano, na uzalendo, na kutimizwa kwa malengo tuliyojiwekea, huleta uendelevu wa maendeleo yetu. Hivyo basi, Serikali itachukua hatua za kimkakati kuweka mazingira rafiki ya kisera, kisheria na kiutendaji yatakayoongeza fursa za biashara, uwekezaji na fursa nyingine za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa Watanzania wote. 

Wakati huohuo, tutaendelea kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi bila kusahau wajibu wetu wa kulinda rasilimali za nchi ili zitumike kwa manufaa ya Taifa. Ndugu Wananchi; Kiungo kingine cha maendeleo ni uwepo wa Utulivu wa Kisiasa na hali ya Amani na Usalama nchini. Mwaka 2025, pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata, tulipitia pia changamoto na mitihani iliyotugusa sote. 

Itakumbukwa kuwa mwezi Oktoba, mwaka huu, tulipitia nyakati ngumu zilizohitaji subira, mshikamano na uzalendo. Kwa dhati kabisa, ninavishukuru Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama nchini, na Wananchi wote kwa ujumla, kwa kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu. Tumeweza kuuthibitishia ulimwengu kwamba Tanzania ni Taifa imara, himilivu na lenye kujitahidi kushughulikia changamoto zake. Tunapouanza mwaka 2026, Serikali imejipanga kujenga umoja wa kitaifa nchini. Hatua za kuunda Tume ya maridhiano zimeanza kuchukuliwa. Serikali itashirikiana na wadau wote katika kukubaliana kuhusu muundo wa Tume, aina ya wajumbe, majukumu yao, na muda wa kazi wa Tume hiyo. 

5 Nitoe rai kwenu ndugu zangu Watanzania, kwamba tunapoendelea kulijenga Taifa letu, tusikubali tofauti za kiitikadi au kimtazamo zitugawe na kutupotezea malengo yetu ya maendeleo na ustawi wa Taifa letu. Sote tunafahamu kuwa, tofauti ni sehemu ya demokrasia, lakini zisitumike kuligawa Taifa la Tanzania. 

Narudia kusema kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni moja tu; ndani ya Jamhuri hio kuna Watanzania, ambao wamejengwa na itikadi ya kuamini kwamba Amani, Umoja na Mshikamano hujenga Uzalendo na ndio virutubisho vinavyotuletea maendeleo endelevu na ustawi wa Watanzania. Ndugu Wananchi; Katika mwaka 2025, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetimiza majukumu yake nchini na hata kikanda na kimataifa.

 Tumeweza kutimiza kikamilifu wajibu wa uanachama wetu katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola (Common Wealth), Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), na vile vile, Umoja wa Mataifa (UN). 

Tumetimiza wajibu wetu wa kulipa ada za uanachama, kushiriki mikutano, kujenga haiba na kuilinda heshima ya Taifa letu, na kutoa mchango wetu kwenye shughuli za kimaendeleo, mazingira, siasa, ulinzi na usalama duniani. Aidha, mwaka 2026 Tanzania itaendelea kuimarisha na kudumisha ushirikiano wa kimataifa na kikanda. Vilevile, Tanzania itaendelea kutumia Diplomasia ya Uchumi kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kujenga ustawi wa watu wake, sambamba na kusimamia ulinzi wa 6 Taifa na mchango wake katika amani na usalama barani Afrika na Duniani kwa ujumla. Ndugu Wananchi;

 Nihitimishe kwa kuwasihi Watanzania wote, tusherehekee sikukuu za kumaliza mwaka na kuanza kwa mwaka unaokuja kwa amani na salama. Baada ya kusema hayo, niwaombe muungane nami tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie Mwaka 2026 uwe wa Kheri na Baraka tele, Amin. Nawatakia kila la Kheri katika Mwaka 2026. Mungu ibariki Afrika! Mungu ibariki nchi yetu Tanzania! Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment