Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni akishuka kwenye ndege baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi.
RAIS wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta
Museveni, amewasili jijini Dar kwa ziara rasmi ya siku mbili kuanzia tarehe 5-6
Agosti 2026, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Rais Museveni pamoja na ujumbe wake amepokelewa katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar Es Salaam na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Mahmoud
Thabit Kombo, pamoja na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu
Fred Mwesigye na viongozi waandamizi wa Serikali.
Akiwa nchini, Rais Museveni anatarajiwa kufanya mazungumzo
rasmi na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar Es Salaam,
yatakayojikita katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, biashara,
uwekezaji, miundombinu na sekta nyingine za kimkakati kwa manufaa ya nchi zote
mbili.
Ziara hii ni ya pili kwa Mheshimiwa Rais Museveni nchini
Tanzania katika mwaka 2026. Ziara yake
yakwanza ilifanyika Februari 2026,
ambapo viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande
mbili, pamoja na utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja
ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) uliofanyika mwezi Machi 2026.
Ziara hii inatarajiwa kutoa msukumo mpya katika utekelezaji
wa maamuzi yaliyokwishafikiwa na kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimkakati kati
ya Tanzania na Uganda kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni akiwasalimia wananchi waliofika kumpokea Uwanja wa Ndege kwa ajili ya ziara ya kikazi nchini.


No comments:
Post a Comment