MASAUNI AITAKA CRDB NA NCMC KUSHIRIKIANA KUCHOCHEA UWEKEZAJI KATIKA MIRADI YA KABONI NCHINI - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 14 November 2026

MASAUNI AITAKA CRDB NA NCMC KUSHIRIKIANA KUCHOCHEA UWEKEZAJI KATIKA MIRADI YA KABONI NCHINI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kushoto aliyesimama) na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi wakishuhudia Mkurugenzi Mtendaji wa NCMC, Bi. Ngenda Kathryn Kigaraba na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB Dkt. Abdulmajid Nsekela wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (wa pili kushoto), Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, Mkurugenzi Mtendaji wa NCMC, Bi. Ngenda Kathryn Kigaraba na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB Dkt. Abdulmajid Nsekela wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU).

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi. Hamad Yussuf Masauni, amezitaka Taasisi za Serikali na sekta binafsi kuimarisha ushirikiano katika kukuza Soko la Biashara ya Kaboni nchini ili kuongeza fursa za uwekezaji wa kijani, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.

Mhe. Masauni ameyasema hayo wakati wa Utiaji Saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya Kituo cha Taifa cha Kuratibu Biashara ya Kaboni (NCMC) na Benki ya CRDB, Novemba 13, 2026, jijini Antalya Uturuki, pembezoni mwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31).

Waziri Masauni amesema lengo nia kushirikiana katika kuendeleza, kufadhili na kutangaza miradi ya kaboni pamoja na kushiriki katika soko la kaboni nchini Tanzania.

Amesema mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoathiri maendeleo endelevu, hivyo kukabiliana nayo kunahitaji sera na mifumo imara ya kisheria, ubunifu katika upatikanaji wa fedha, ushiriki wa sekta binafsi na ushirikiano wa kimkakati baina ya wadau mbalimbali.

Ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeitambua sekta ya soko la kaboni kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya mageuzi ya kiuchumi, yanayoweza kusaidia kuhamasisha upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuvutia uwekezaji wa kijani na kuchangia maendeleo ya uchumi.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha biashara ya kaboni haiishii katika kuzalisha na kuuza hati za kaboni pekee, bali inazalisha manufaa halisi ya kiuchumi, kijamii na kimazingira, ikiwemo kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza ajira, kuhamisha teknolojia na kuongeza ushiriki wa jamii na wafanyabiashara wa Kitanzania,” amesema Mhe. Masauni.

Katika hatua nyingine, ameitaka CRDB kuendelea kubuni mifumo mbalimbali ya kifedha ikiwemo mikopo, dhamana na nyenzo nyingine za uwekezaji zitakazowezesha wamiliki na waendelezaji wa miradi ya kaboni kupata mitaji kwa kuzingatia tathmini za benki na matakwa ya kisheria.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NCMC, Bi. Ngenda Kathryn Kigaraba, amesema hatua ya ushirikiano huo katika maendeleo ya soko la Biashara ya kaboni nchini utawezesha miradi ya kaboni kupata mitaji kutoka ndani ya nchi.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela ameeleza kuwa ushirikiano huo utafungua fursa za uwekezaji, kuvutia mitaji na kuwezesha miradi ya kaboni yenye manufaaa kwa uchumi na jamii.

Akiongea awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt.Richard Muyungi amefafanua kuwa ushirikiano huo utawezesha utekelezaji wa Dira ya 20250 ambapo sekta ya biashara ya kaboni inaweza kuwa miongoni mwa nyenzo za kuvutia uwekezaji na kuchochea shughuli za uzalishaji.

No comments:

Post a Comment