BARAZA la Mawaziri wa Usafirishaji wa nchi wanachama wa ushoroba wa kati (Central Corridor) imeikabidhi Tanzania kuwa Mwenyekiti kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia Mwaka 2021 hadi 2022.
Uwenyekiti huo umekabidhiwa jijini Dar es Salaam kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho kutoka kwa Waziri wa Miundombinu wa Rwanda Mheshimiwa Balozi Claver Gatete katika kikao chao cha 11 kilichofanyika kwa njia ya mtandao.
Dkt. Chamuriho amekabidhiwa Uwenyekiti huo katika kikao hicho kinachojumuisha mawaziri wa usafirishaji kutoka nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Tanzania ambazo ni nchi wananchama wa Taasisi ya Ushoroba wa Kati yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho mawaziri wamekubaliana kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya nchi wanachama kwa kujenga na kuimarisha usafiri katika Sekta ya Maji, Reli, Barabara na kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam inaboreshwa zaidi ili kuondoa ucheleweshaji wa shehena ya mizigo kwenda nchi wananchama.
Aidha, umoja huo pia umezindua mpango mkakati wa taasisi wa Ushoroba wa kati wa miaka mitano (2021 -2025) ambao utaangazia njia zote za usafirishaji (maji, reli na barabara) pamoja na miundombinu husika kwa kusimamia, kuimarisha, kuongeza ushindani, kuboresha pamoja na masuala mengine ya uratibu na ufuatiliaji.
Baadhi ya miradi iliyoingizwa katika mpango huu ni ujenzi wa reli ya kisasa SGR kipande cha Uvinza-Musongati (km 240), ujenzi na ukarabati wa Bandari za Bujumbura, Rumonge na Kabonga nchini Burundi na na ujenzi wa barabara ya kimataifa kati ya Tanzania na Burundi (Rumonge-Gitaza-Kabingo-Kasulu-Manyovu)
Miradi mingine ni pamoja na reli ya kisasa kutoka Isaka hadi Kigali, ujenzi wa mizani za kupimia mizigo nchini Rwanda, ujenzi na ukarabati wa bandari mbalimbali nchini DRC, ujenzi wa meli ya mizigo kwenye Ziwa Victoria.
Katika hotuba yake Dkt. Chamuriho ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshasaini mikataba mitano ya ujenzi na ukarabati wa meli.
"Serikali imeshaingia makubaliano ya ujenzi na ukarabati wa meli hizo ambao utaanza hivi karibuni kwa ajili ya kutoa huduma katika katika Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria na Bahari ya Hindi, ikiwa ni jitihada za kuimarisha usafirishaji katika Ushoroba wa Kati", alifafanua Dkt. Chamuriho.
Kuhusu usafirishaji wa njia ya reli, Dkt. Chamuriho, ameeleza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa sehemu ya Mwanza hadi Isaka umeshaanza na unatarajiwa kukamilika mapema mwaka 2024.
"Kwa upande wa maendeleo ya ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa, kipande cha kwanza kati Dar es Salaam hadi Morogoro ujenzi umefikia asilimia 92 na kipande cha Morogoro hadi Makutupora ujenzi umefikia asilimia 65", alifafanua Dkt. Chamuriho.
Kabala ya kikao cha Mawaziri wa nchi wananchama kulitanguliwa na kikao cha Makatibu wakuu wa nchi wananchama ambapo Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Bw. Gabriel Migire.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
No comments:
Post a Comment