WAKAGUZI wa Ndani wa Serikali wameaswa kutazamia upya athari za mabadiliko ya kimazingira pindi wanapofanya ukaguzi katika masuala ya Mazingira, Kijamii na Utawala Bora (Environmental, Social, and Governance-ESG) na Ukaguzi wa Thamani ya Fedha (Value for Money-VFM) kwenye Miradi ya Maendeleo, ili kuboresha ufanisi na ustawi endelevu wa miradi ya maendeleo katika taifa na kupunguza kasi ya athari ya Mabadiliko ya Mazingira.
Hayo yamesemwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (IAG), Bw. Benjamin Magai, alipokuwa anafungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi na Wakaguzi Wakuu wa Ndani kutoka katika Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri na Taasisi mbalimbali za Serikali zipatazo 90, katika masuala muhimu ya Ukaguzi wa Mazingira, Kijamii na Utawala Bora pamoja na Ukaguzi wa Thamani ya Fedha kwenye Miradi ya Maendeleo, yaliyofanyika katika ukumbi wa Cate Hotel, mjini Morogoro.
Bw. Magai alisema kuwa, hivi sasa ulimwenguni kote masuala ya Mazingira, Kijamii na Utawala Bora pamoja Ukaguzi wa Thamani ya Fedha kwenye Miradi ya Maendeleo, ni maeneo mapya na muhimu katika kutekeleza majukumu ya kusimamia miradi hasa eneo la ukaguzi wa unaohusu ESG (Mazingira, Kijamii na Utawala Bora) ambalo limekuwa likipigiwa kelele nyingi Kitaifa na hata Kimataifa.
Alisema kuwa miradi mingi kwasasa inayofadhiliwa na Washirika wa Maendeleo imekuwa ikisisitizwa kuzingatia masuala ya mazingira, kijamii na Utawala bora ikiwa ni sehemu muhimu kwa sababu miradi ya maendeleo inaweza kuathiriwa na masuala ya mazingira, kijamii, na utawala bora; na wanapaswa kuhakikisha kwamba rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Katika mafunzo haya, nina imani mtapata maarifa na ujuzi wa jinsi ya kufanya ukaguzi na jinsi ya kutambua na kudhibiti hatari zinazohatarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Pia, mtajifunza jinsi ya kutumia mbinu na zana za kisasa za ukaguzi ili kuboresha ufanisi na ustawi endelevu wa miradi ya maendeleo katika Taasisi zetu tunazotoka” alisema Bw. Magai
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanaangazia maeneo mengine zaidi ikiwemo Ukaguzi na Tathmini ya Athari kwa Mazingira; Tathmini ya Mazingira Kimkakati; Athari za Mabadiliko ya Tabianchi na juhudi za kitaifa na kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, lakini pia, majadiliano kuhusu fursa zilizopo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo biashara ya kaboni na faida zake kijamii, kiuchumi na kisiasa sambamba na ukaguzi wa Thamani ya Fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Sote tunafahamu kuwa tasnia ya ukaguzi wa ndani ni jicho muhimu sana la Serikali katika kubaini na kuibua kasoro za kiutendaji, usimamizi wa rasilimali za nchi na kushauri Serikali ipasavyo, Hivyo, mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani ili waweze kufanya ukaguzi wa kina na wa uhakika kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vigezo vya ESG na VFM” alisema Bw. Magai
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, Bw. Jackson Kingumwile aliishukuru Wizara ya Fedha kuandaa mafunzo hayo kwa kuwa yatasaidia kuharakisha utunzaji wa mazingira sambamba na kufikia malengo ya Serikali na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs-2030) ya Umoja wa Mataifa.
Bw. Kidumule alisema kuwa, wakaguzi watatoka wakiwa na uelewa mpana katika kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakaguliwa ipasavyo ili kuhakikisha haiathiri mazingira ili kulinda ekolojia nchini.
“Wakaguzi na wadau wa mazingira wazingatie nakuhakikisha kwamba miradi inatunza mazingira ili ustawi wa jamii na Uchumi uwe chanya kwa maendeleo ya Taifa letu” aliongeza Bw. Kingumwile
Mafunzo haya yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika tasnia ya ukaguzi wa ndani, kwa kuwaongezea wakaguzi uwezo wa kuchambua kwa kina masuala ya mazingira, kijamii na utawala bora katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo kupitia uelewa huo mpya, Serikali inatarajia kuona uwajibikaji mkubwa zaidi, matumizi bora ya rasilimali za umma, na miradi yenye tija kwa wananchi huku ikilinda mazingira na kuendeleza ustawi wa kijamii.


No comments:
Post a Comment