MSOFE AWACHARUKIA WAWEKEZAJI, AWATAKA WALIPE KODI - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 16 August 2026

MSOFE AWACHARUKIA WAWEKEZAJI, AWATAKA WALIPE KODI

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ilala, Mohammed Msofe, akizungumza na wawekezaji waliowekeza katika  flemu za maduka huko Zingiziwa, jijini Dar es Salaam Agosti 15, 2026.

 Na Mwandishi Wetu. 

 MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi   (CCM), Wilaya ya Ilala, Mohammed Msofe, amecharuka, baada ya kuwataka wawekezaji wa flemu za maduka kuanza kulipa kodi ili pande zote mbili ziweze kunufaika na mapato. 

Msofe alisema hayo Agosti 15, mwaka huu, wakati akizungumza na wawekezaji katika Kata ya Zingiziwa, Ilala, jijini Dar es Salaam. 

Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na Kamati ya Utekezaji Wazazi CCM Wilaya ya Ilala, alisema kuwa kitendo cha wawekezaji hao kuendelea kukaa bure bila kulipa kodi ni kuinyima jumuiya hiyo  mapato.

"Nataka wawekezaji wanaofanya biashara katika eneo hili, kufika ofisini ili  tuweze kuweka utaratibu wa kukubaliana namna ya kulipa kodi," alisema Msofe.

Msofe alisema kuwa haiwezekani wawekezaji hao waendelee kukaa bure   katika flemu hizo bila kulipa kodi, kwani wanarudisha nyuma maendeleo  ya jumuiya ya wazazi CCM. 

Wawekezaji hao ambao wana muda wa zaidi ya miaka tisa kuanzia mwaka 2018, Msofe alisema kuwa ifike wakati sasa waanze kulipa kodi bila kujali mwenye flemu ameanza kufanya biashara au la.               

Mwenyekiti huyo alisema kuwa anataka kuona kila mwekezaji ambaye atafanyabiashara katika eneo lao lililopo Zingiziwa anazingatia utaratibu wa kulipa kodi.

"Haiwezekani upande mmoja unufaike wakati mwingine haupati mapato yoyote, tunarudisha nyuma jumuiya," alisema.

Kamati hiyo ya Utekelezaji chini ya Msofe ilipata nafasi ya kuongea na wawekezaji kwa lengo la kujua changamoto zinazokwamisha uendelezaji wa ujenzi wa flemu za maduka katika eneo hilo.             Baadhi ya wawekezaji hao walisema kuwa changamoto zilizokuwapo ni pamoja na mgogoro wa ardhi katika eneo hilo.

Mmoja wa wawekezaji hao, Manufred Ndunguru alisema kuwa sababu hiyo iliwafanya washindwe kuendelea na uwekezaji.  

Akijibu hoja za wawekezaji hao, Msofe alisema kuwa eneo hilo kwa sasa ni salama na halina mgogoro wowote.

Msofe alisema kuwa eneo hilo ambalo linamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Ilala, limepimwa na tayari limepandwa mawe, hivyo lipo salama.

Pamoja na kamati hiyo kuzungumza na wawekezaji walipanga kukutana kwa mara nyingine  Septemba 5, mwaka huu.

Msofe amewataka viongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM  Kata ya Zingiziwa, akiwamo mwenyekiti, mweka hazina na wawekezaji kufika katika mkutano huo, ambao utakuwa wa kuweka utaratibu wa uwekezaji katika eneo hilo.

Pia,  kamati ya utekelezaji ya jumuiya hiyo iliweza kutembea nyumba ya mtumishi inayoendelea kujengwa katika eneo hilo.  

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ilala, Mohammed Msofe, akisisitiza jambo wakati akizungumza na wawekezaji waliowekeza katika flemu za maduka katika Kata ya Zingiziwa.
Ziara katika Kata ya Zingiziwa ikiendelea. 

No comments:

Post a Comment