Na Benny Mwaipaja, Tunduma
WAZIRI wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewahakikishia wakazi wa Mji wa Tunduma, Wilayani Momba mkoani Songwe kwamba Serikali itatoa fedha sh. bil. 17 kwa ajili ya mradi wa kusambaza maji katika mji huo kutoka chanzo cha maji cha Mto Bupigu, kilichoko Wilaya ya Ileje.
Dkt. Nchemba alisema hayo Mjini Tunduma wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji huo wakiwemo wafanyabiashara katika Mpaka huo wa Tanzania na Zambia.
"Mama yetu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumtua ndoo mama kichwani kwa kuipa kipaumbele sekta ya maji, nimepokea maelezo yenu sisi watendaji wake ni kutekeleza ahadi alizowaahidi" Alisema Dkt. Nchemba.
Alifafanua kuwa Wizara itahakikisha inatoa kiasi hicho cha fedha ili wananchi hao wapate maji na kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa maji mijini unafikia wastani wa asilimka 95 na vijijini asilimia 85.
*Kuhusu kupanda kwa bei ya mbolea*
Dkt. Nchemba aliwajibu wananchi hao waliolalamikia kupanda kwa bei ya mbolea kwamba Serikali inalifanyiakazi suala la kupanda kwa bei hiyo na kwamba wataalam wa Sekta ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango wanapitia na kuyafanyiakazi masuala mbalimbali ya kisera yatakayosaidia kupungua kwa bei hiyo.
"Kupanda kwa bei ya mbolea hakutokani na kodi na tozo zilizoongezwa kwenye bajeti hii bali inatokana na kupanda kwa bei huko inakozalishwa nje ya nchi" Alisisitiza Mhe. Nchemba
*Kuhusu wafanyabiashara wa Tanzania kuhamia Zambia*
Aliwataka wafanyabiashara hao kurejea na kufanyabiashara nchini na kuwahakikishia kuwa malalamiko yao kuhusu kodi yatafanyiwakazi. Wito huo ulitokana na baadhi ya wafanyabiashara kueleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wenzao wamehamishia biashara zao upande wa Nakonde nchini Zambia wakidai kuwa kufanya biashara upande huo kuna nafuu ya kodi ikilinganishwa na upande wa Tanzania.
“Wewe ni Mtanzania usiikimbie nchi yako, tutarekebisha matatizo, lakini kama umepata fursa ya kuwekeza huko, wekeza! Laniki usiikimbie nchi yako kwa sababu ya matatizo. Tanzania inaheshima ya kuzikomboa nchi zote hizi hatuwezi kushindwa kutenda haki kwa wananchi wetu” Aliongeza Dkt. Nchemba
Akutana na TRA na Wafanya Biashara
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kuweka utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara mara kwa mara ili kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kutoa stakabadhi za kielektroniki zikiwa na bei halali.
Aliwaonya pia wafanyabiashara kuacha tabia ya kuuza huduma na bidhaa zao kwa kutumia bei za aina mbili; moja ikiwa ni kuwauzia wateja bidhaa bila kutoa risiti au kuandika kiasi kisichosahihi akibainisha kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kwamba wakikamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akitoa taarifa ya utendaji, Meneja wa TRA mkoa wa Songwe Bw. John Micah alisema kuwa Mamlaka yake imefanikiwa kuvuka malengo ya ukusanyaji kodi ambapo katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2020/2021 walikusanya sh. bil. 92.7 sawa na ufanisi wa asilimia 115 ikilinganishwa na lengo walilowekewa la kukusanya sh. bil. 80.3.
Kwa upande wa wafanyabiashara, waliiomba Serikali kuhuisha masuala ya kodi ili waweze kulipa kodi kwa mamlaka moja badala ya kila taasisi kudai kodi na tozo mbalimbali jambo walilosema linawaletea usumbufu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba yuko ziarani mkoani Songwe kukagua shughuli za maendeleo zinazohusiana na Wizara yake ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wafanyabiashara.
No comments:
Post a Comment