WAHANDISI WATAKIWA KUENDANA NA KASI YA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 5 September 2024

WAHANDISI WATAKIWA KUENDANA NA KASI YA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA

 

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Mhandisi Wakili Menye Manga wakati wa Maadhimisho ya 21 ya Siku ya Wahandisi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 05, 2024.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza wakati akifungua Maadhimisho ya 21 ya Siku ya Wahandisi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 05, 2024.

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa rai kwa Wahandisi nchini kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia mbalimbali ikiwemo ya Akili Mnemba kutoa suluhu ya changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.

Bashungwa ameeleza hayo leo Septemba 05, 2024 jijini Dar es salaam wakati akifungua Maadhimisho ya 21 ya Siku ya Wahandisi iliyobeba kauli mbiu “Kuandaa Nguvukazi ya Uhandisi katika zama za Akili Mnemba - Mafunzo na Kuimarisha Ujuzi wa Watalaam wa Kada ya Uhandisi”.

“Tumieni fursa hii kutafakari changamoto mbalimbali za shughuli za kihandisi zenye mahusiano ya moja kwa moja na maendeleo ya nchi yetu, badilishaneni mawazo na kuona ni teknolojia ipi itasaidia kutatua changamoto”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wanatoa fursa ya ujenzi wa madaraja na makalvati ya yaliyoharibiwa na mvua za El-Nino ambazo tayari kiasi cha shilingi Bilioni 840 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wake kwa Wakandarasi na Washauri Elekezi Wazawa.

“Hakikisha kila mradi unachukua wanafunzi wawili katika miradi 114 ya kurejesha miundombinu iliyoyahiribiwa mikoa yote nchini, hii itasaidia kuinua vijana na kuwajengea uwezo”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ametoa rai kwa wahandisi na wataalam wote wazawa kujiamini na kufanya kazi kwa uaminifu, Kizalendo, kukamilisha miradi kwa wakati na kuzingatia miiko na viapo vya kihandisii walivyoapa ili kuepusha masuala ya ongezeko la gharama katika miradi na miradi kuharibika kabla ya wakati.

Aidha, Bashungwa ameielekeza TANROADS kuhakikisha wanafanya mapitio ya usanifu kabla ya kutangaza zabuni kwa miradi ambayo usanifu wake umefanyika miaka mingi iliyopita.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Aisha Amour ameeleza kuwa kila mwaka Wizara inatenga kiasi cha shilingi Milioni 788 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya wahandisi wahitimu (SEAP) ili kuwajengea uwezo.

Akitoa taarifa ya Bodi, Msajili wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Mhandisi Bernad Kavishe ameeleza kuwa hadi kufikia Julai 31, 2024 Bodi imesajili Wahandisi 39,236 katika ngazi mbalimbali za usajili ambapo kati ya hao Wahandisi Wanawake ni 5,276, Mafundi Sanifu 2,976, Kampuni za Ushauri wa Kihandisi 431 na Maabara 52.

Maadhimisho ya 21 ya Siku ya Wahandisi yamehudhuriwa na takriban Wahandisi 4,000 huku zaidi ya wahandisi 300 wakila kiapo cha utii cha Uhandisi.

No comments:

Post a Comment