RAIS MWINYI ASISITIZA JUHUDI KATIKA KUTATUA MGOGORO WA DRC - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 20 November 2024

RAIS MWINYI ASISITIZA JUHUDI KATIKA KUTATUA MGOGORO WA DRC

 


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ally Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ally Mwinyi, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC ORGAN TROIKA SUMMIT) uliofanyika jijini Harare, Zimbabwe tarehe 20 Novemba 2024.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi ulijadili hali ya amani na usalama Mashariki mwa Nchi ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mkutano huo ulitanguliwa na vikao pamoja na mikutano ya Kamati na Mabaraza katika Ngazi ya Makatibu Wakuu na Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Rais Mwinyi amewataka Wakuu wa Nchi kuongeza juhudi katika kutatua mgogoro wa muda mrefu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC ). 

Akizungumza katika Mkutano huo, Amesema Tanzania kama Mwenyekiti wa Asasi ya SADC inatambua umuhimu wa uwepo wa amani, ulinzi na usalama maana ndio kichocheo katika Ukuaji wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii hivyo hatuna budi kuhakikisha tunaweka jitihada za makusudi katika kutatua mgogoro Mashariki mwa Kongo.

" Pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikumba kanda ikiwemo hali ya kifedha bado tuna jukumu la kuunganisha nguvu ya pamoja kwa kuchangia rasilimali ili kufanikisha maazimio yetu ya kuleta Suluhu ya kudumu DRC. 

" Ni azma ya Nchi na Kanda kuona tunaunga mkono juhudi za Kidiplomasia za kumaliza uhasama kati ya Kongo na Rwanda chini ya Usimamizi wa Angola na Misheni ya Kijeshi ya SAMIDRC." alisema Rais Mwinyi.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

No comments:

Post a Comment