WATHAMINI WAPATIWA MAFUNZO UANDAAJI VITALU VYA THAMANI YA ARDHI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 16 December 2024

WATHAMINI WAPATIWA MAFUNZO UANDAAJI VITALU VYA THAMANI YA ARDHI

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kilimanjaro Bi. Rehema Jato akifungua mafunzo ya uandaaji vitalu vya thamani ya ardhi kwa wathamini na warasimu ramani mkoa wa Kilimanjaro tarehe 16 Disemba 2024.

Na Munir Shemweta, KILIMANJARO

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini (LTIP) imetoa mafunzo kwa Wathamini na Warasimu Ramani kwa ajili ya zoezi la Uandaaji Vitalu vya Thamani ya Ardhi (Valuation Block)

 

Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza leo tarehe 16 Disemba 2024 na yanahusisha wataalamu wa fani ya Uthamini na Urasimu Ramani kutoka ofisi ya Kamishna wa Ardhi mkoa wa Kilimanjaro pamoja na halmashauri zote za mkoa huo.

 

Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye ni Mthamini kutoka Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali Bw. Baraka Mollel amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha na kuwafundisha wathamini na warasimu ramani ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hasa kipindi hiki ambacho Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaboresha mifumo yake na kuwa ya kidigitali.

 

Ameongeza kuwa, mafunzo hayo yanawafundisha wathamini na warasimu ramani namna ya kuandaa Vitalu vya Thamani ya Ardhi (Valution Block) ili kusaidia utekelezaji wa shughuli za uthamini kama vile Rehani, Uhamishaji Milki na Uthamani kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya serikali.

 

"Uandaaji Vitalu vya Thamani kwa Wathamini na Warasimu Ramani utajumuishwa kwenye mfumo wa e-ardhi utakaowezesha ukilaji tozo mbalimbali ikiwemo kodi ya ardhi na tozo nyingine zitokanazo na thamani" amesema Bw. Mollel.

 

Ametaja faida ya Vitalu vya Thamani ya Ardhi (Valutaion Block) kuwa, ni kuiwezesha wizara katika makusanyo ya kodi ya ardhi, miamala mbalimbali ya uthamini pamoja na tozo nyingine kama vile tozo ya mbele hivyo wanatoa mafunzo namna ya kuandaa vitalu na kuwaelekeza namna ya kuunganisha katika mfumo wa e-ardhi.

 

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kilimanjaro Bi. Rehema Jato ameishukuru Wizara Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuona umuhimu wa kuupa mkoa wake kipaumbele cha kupata mafunzo hayo aliyoyaeleza kuwa ni muhimu sana kwa wathamini na warasimu ramani katika mkoa huo.

 

‘’Tunajua kuwa mafunzo haya yataenda mikoa yote lakini angalau sisi Kilimanjaro tumekuwa watu wa mwanzo mwanzo hivyo tuyatumie mafunzo haya katika kuongeza ujuzi na hatimaye kufikia malengo’’ amesema Rehema

 

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza matumizi ya mifumo ya kidigitali (e-ardhi) ambapo hivi karibuni Waziri wake Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanatumia mifumo ya teknolojia katika yale maeneo ambayo mfumo huo umeanza kutumika.

 

Mfumo wa e-Ardhi umeanza kutumika kwenye maeneo mbalimbali nchini kama vile Dodoma, Arusha, Tabora katika halmashauri ya Nzega, Pwani halmashauri ya Chalinze pamoja na manispaa ya Shinyanga na Kahama zilizopo mkoa wa Shinyanga.

No comments:

Post a Comment