TANZANIA YAVIVUNIA KAMPUNI YA BAKHRESA KWA ULIPAJI WA KODI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 17 December 2024

TANZANIA YAVIVUNIA KAMPUNI YA BAKHRESA KWA ULIPAJI WA KODI

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, akihutubia wakati akizindua muonekano mpya wa juisi ya African Fruti inayotengenezwa na Kampuni ya Bakhresa Group katika hafla iliyofanyika Hyatt Hoteli Desemba 16, 2024 jijini Dar es Salaam.

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania inajivunia kwa kuwa na Kampuni ya Bakhresa Group ambayo imefanya uwekezaji mkubwa  nchini na imekuwa mlipaji mzuri wa kodi.

Dkt. Jafo ambaye alikuwa mgeni rasmi ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa muonekano mpya wa juisi ya African Fruti inayotengenezwa na kampuni hiyo kwenye uzinduzi uliofanyika Hyatt Hoteli Desemba 16, 2024.

“ Katika makampuni makubwa Tanzania inajivunia Kampuni ya Bakhrea kwa ulipaji wa kodi na kuweka rekodi hiyo,” alisema Jafo huku akishangiliwa.

Alisemma kampuni hiyo imeweka uwekezaji mkubwa wa Sh. Bilioni 700 kwa ajili ya kununua mashine mpya za kuchakata bidhaa za mazao jambo ambalo ni kubwa.

Aidha Dkt. Jafo aliitaka kampuni hiyo kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha matunda yanayostawi kwa muda mfupi ili kuwezesha bidhaa hiyo kupatikana kwa wingi kwa ajili ya uzalishaji wa vinywaji hivyo ambapo aliwaomba vijana kuchangamkia fursa ya kilimo hicho chenye soko la uhakika.

Dkt. Jafo alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya ya kutengeneza miundombinu ya barabara ili bidhaa hizo zinazozalishwa hapa nchini ziweze kufika kufika kila sehemu.

Alisema hivi sasa kila mahali kuna ujenzi wa barabara ukiendelea na sasa kasi kubwa ikifanyika Mkoa wa Kigoma lengo ni kuifungua nchi kibishara.

Alisema ujenzi wa Reli ya SGR unakwenda kukuza biashara na kuunganisha nchi za Rwanda, Burundi na DRC Kongo ambazo hazina Bandari.

Akizungumzia kazi nyingine kubwa iliyofanywa na Serikali ni ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere ambapo zaidi ya Sh. Trioni 6.5 zilitengwa na shabaha kubwa ni kuzalisha nishati ya umeme ili viwanda viweze kufanya kazi ya uzalisha kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa BFPL, Salim Aziz alimshukuru Dkt. Jafo kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambapo alisema maagizo yake yote aliyoyatoa watayatekeleza na akatoa shukurani kwa watanzania kuendelea kuiunga mkono kampuni hiyo kwa kununua bidhaa zao.

No comments:

Post a Comment