Kazi za ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga zikiendelea ambapo kwa sasa kazi zinazofanyika ni pamoja kuweka tabaka la lami kwenye eneo la maegesho ya ndege na eneo la kuingia na kutokea ndege.
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya amemuagiza Mkandarasi China Henan International Cooperation (CHICO) anayejenga mradi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga kuhakikisha anakamilisha mradi huo ifikapo Aprili 2025.
Akizungumza mkoani Shinyanga Desemba 18, 2024 mara baada ya kukagua mradi huo na kuridhishwa na maendeleo yake Kasekenya amesisitiza Mkandarasi huyo kuhakikisha anaongeza nguvu kazi na kufanya kazi usiku na mchana ili kufikia lengo kwa mujibu wa mkataba.
"Maendeleo ya mradi ni mazuri mpaka sasa, kikubwa fanyeni kazi usiku na mchana, ongezeni wafanyakazi pamoja na vifaa ili kuongeza kasi ya ujenzi, hata jengo la abiria nalo likamilike kwa wakati", amesema Kasekenya
Kasekenya ameagiza pia Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga na Mhandisi Mshauri SMEC kuhakikisha wanamsimamia kwa karibu Mkandarasi huyo kujenga mradi huo kwa viwango na ubora na kukamilisha mradi kwa wakati.
Aidha, Kasekenya amesema kuwa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga ni muhimu kwani ukikamilika utakuwa kiunganishi muhimu kwa maeneo ya Ukanda wa ziwa hasa wakazi wa Shinyanga na maeneo jirani.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na kuahidi watasimamia mradi huo na kuhakikisha unakamilika na kukabidhiwa kwa wakati kwani kukamilika kwake utaleta maendeleo na kukuza uchumi Mkoani Shinyanga.
Awali akitoa Taarifa ya Mradi, Mhandisi Mshauri kutoka SMEC Gosbert Ruburi, amesema kuwa kazi zinazoendelea kufanyika ni pamoja na ujenzi wa tabaka la lami kwenye eneo la kuingia na kutokea ndege na eneo la maegesho ya ndege pamoja na ujenzi wa jengo la abiria.
Aidha, Mhandisi Ruburi amefafanua kuwa hadi sasa mradi huo umetoa jumla ya ajira 160 ambapo kati ya ajira hizo asilimia 80 ni kwa watanzania.
Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyannga wenye urefu wa Kilometa 2.2 unafadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo ni moja ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mkoa huo na mikoa jirani.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.
No comments:
Post a Comment