WAZIRI SILAA AZINDUWA BODI YA SHIRIKA LA MAWASILIANO TANZANIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 17 December 2024

WAZIRI SILAA AZINDUWA BODI YA SHIRIKA LA MAWASILIANO TANZANIA

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (kulia) akimpongea Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TTCL, Bw. David Nchimbi mara baada ya kuzindua bodi hiyo.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TTCL, Bw. David Nchimbi mara baada ya kuzindua bodi hiyo.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), amezinduwa rasmi Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), huku akiitaka bodi hiyo kuandaa mpango kazi utakaowezesha shirika hilo kujiendesha kibiashara.

Waziri, Mhe. Silaa (Mb) ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Shirika la TTCL, pamoja na kuikabidhi bodi hiyo vitendea kazi kabla ya kuanza kazi yake.

Amesema kuwa maagizo aliyoyatoa katika bodi hiyo, ni sehemu ya maelekezo mahsusi yaliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Desemba 10, 2024, Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar kwenye hafla ya uapisho wa Mawaziri, Naibu Mawaziri na viongozi mbalimbali. Rais alisema TTCL inatakiwa kujiendesha kibiashara ili kufikia malengo yake.

Waziri Silaa amesema, "Serikali ya Rais Dkt. Samia imewekeza fedha nyingi katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo mkongo wa taifa wa mawasiliano, minara ya mawasiliano, pamoja na kituo cha kuhifadhia data cha taifa (National Data Center).

"Nia ya Rais ni kuona uwekezaji huu mkubwa unaleta tija nchini." Amesema Waziri Silaa na kuongeza;

"Shirika hili likiendeshwa vyema lina uwezo wa kusaidia sekta nyingine, kwa sababu wizara yetu ni wezeshi katika mawasiliano, hivyo wizara nyingine na Taasisi zinaitegemea katika kukuza sekta zao za TEHAMA."

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TTCL, Bw. David Nchimbi akizungumza mara baada ya kukabidhiwa vitendea kazi, amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua kuongoza bodi hiyo na kuahidi kusimamia shirika ili liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Bw. Nchimbi amemshukuru Waziri Silaa kwa utayari alioonesha na kuahidi kuwa bodi itatoa ushirikiano kwa wizara wakati wote itakapokuwa inatekeleza majukumu yake.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi rasmi wa bodi hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TTCL, Bw. David Nchimbi akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) mara baada ya kukabidhiwa vitendea kazi.

Sehemu ya wajumbe wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi rasmi wa bodi hiyo.


No comments:

Post a Comment