MEYA ATAKA WANANCHI WAFAIDI KITUO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 7 August 2023

MEYA ATAKA WANANCHI WAFAIDI KITUO




Na Mwandishi WETU

MEYA wa Jiji la Dar Es Salaam, Omar Kumbilamoto amewaita wananachi wa Mwanagati wilayani Ilala kutumia fursa mbalimbali za kibiashara na kiuchumi zilizo katika Kituo cha Mafuta cha Davida huku pia wakinufaika kwa ajira na huduma mbalimbali.

Katika hafla ya uzinduzi wa Davida Oil uliofanyika Kwampalange Mwanagati wilayani Ilala juzi, Kumbilamoto alisema licha ya kusogeza huduma kwa jamii, pia kituo kitachangia upatikanaji wa ajira rasmi na zisizo rasmi pamoja na kuongeza usalama katika eneo hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Davida Oil, Julius Makere aliapa kuwa suala la huduma bora, uadilifu na uaminifu litakuwa kipaumbele katika uendeshaji na utoaji huduma katika kituo hicho.

Kumbilamoto aliutaka uongozi wa Davida Oil kuweka utaratibu utakaowezesha waendesha bodaboda kufanya biashara zao bila kusababisha adha kwa watumiaji wengine wa eneo hilo.

"Mjue kuwa uwepo wa kituo hiki sasa utachochea na kuongeza usalama katikà eneo hili maana hakutakuwa na mambo ya watu kukabwa hapa... Kituo Cha Davida kimeleta fursa nyingi za kibiashara na kiuchumi sasa mzitumie vizuri na mkichukulie kuwa ni chenu," alisema.

Aliongeza: "Kituo hiki kitasaidia hata serikali kupambana na ukosefu wa ajira maana kama kitatoa ajira zaidi ya 10 kwa kazi za mafuta tu, na bado nyingine hao walioajiriwa wana watu wengi nyuma yao wanaowategemea hivyo, hili ni jema Kwa taifa."

Aliupongeza uongozi wa  kituo hicho kwa kuandaa na kugawa sare na viakisi mwanga kwa bodaboda wa maeneo ya  Mbagala na Buza (Temeke) pamoja na Nyantira, Kwampalange, Kwamamakibonge na Mwangati (Ilala) waliokusanyika katika eneo hilo.

Aidha, bodaboda hao walipewa ofa ya lita moja ya mafuta kwa kila aliyenunua litaa mbili huku pia madereva mbalimbali wa magari wakipata ofa ya namna hiyo.

Akizungumzia changamoto ya miundombinu ya barabara iliyotajwa na Makere katika risala, Meya Kumbilamoto alisema wiki ijayo wataalaamu watafika kuona namna ya kuweka mzunguko wa barabara maarufu round-about, Ili kuwezesha mpishano mzuri wa magari kuingia na kutoka kituoni.

No comments:

Post a Comment