MAANDALIZI YA UZINDUZI WA AFRICAN FOOTBALL LEAGUE YAANZA RASMI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 7 August 2023

MAANDALIZI YA UZINDUZI WA AFRICAN FOOTBALL LEAGUE YAANZA RASMI





Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amepokea ugeni wa timu ya wataalam African Football League chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ili kuanza maandalizi ya ufunguzi rasmi wa mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Oktoba 20, 2023 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya ziara ya ukaguzi wa maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati ili kuendana miongozo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) Agosti 7, 2023 jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema mazungumzo yao yalijikita zaidi kuangalia ubora wa Uwanja na maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati.

“Mazungumzo yetu yalijikita zaidi pamoja na ziara ya uwanja kuangalia ubora wa uwanja na maeneo ambayo tunaenda kuyafanyia ukarabati na mahitaji yao kwa ajili ya mechi ya ufunguzi ambayo kwa bara zima la Afrika itafanyika hapa katika uwanja huu wa Benjamin Mkapa” amesema Katibu Mkuu Bw. Yakubu.

Mashindano African Football League yanatarajiwa kuwa na manufaa mengi kiuchumi hapa nchini kwa kuwaleta wageni mashuhuri takriban 400 ambao watashiriki wakiwemo viongozi wa juu wa CAF na FIFA.

Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema wizara hiyo tayari imeshaingia mkataba na mkandarasi ambapo mkandarasi huyo wa ukarabati huo ni Beijing Construction Engineering Group Co., Ltd. (BCEG) na kusisitiza kuwa mkandarasi huyo amekabidhiwa rasmi uwanja ili aendelee na majukumu yake ya ukarabati.

Ukarabati wa awali utajumuisha masuala mbalimbali ambayo CAF wanahitaji yafanyiwe kazi mapema, baadhi yanagharamiwa ikiwa ni sehemu ya mkataba na baadhi ni gharama inayotolewa na CAF kwa ajili ya mechi hiyo ya ufunguzi ambayo itafanyika nchini.

Kwa hivi sasa mpaka Oktoba 20, 2023 hakutakuwa na mechi nyingine itakayochezwa kwenye uwanja huu wa Benjamin Mkapa ili kupisha maandalizi kwa sababu miongoni mwa vitu watakavyofanya African Football League ni pamoja na kufumua eneo la kuchezea mpira kwa gharama zao na watalirejesha kwenye hali ambayo unachezeka mpira.

Michuano hiyo inashirikisha vilabu nane kote barani Afrika ambapo kwa upande wa Afrika Mshariki, timu ya Simba ya Tanzania ndiyo mwakilishi pekee wa Afrika Mashariki kwenye mashindano hayo ya Afrika ambayo yanachezwa kwa mara ya kwanza kwa kushirikisha timu nane za Afrika.

Aidha, Bw. Yakubu ameongeza kuwa timu za Tanzania ambazo zimefuzu kucheza mashindano yanayoandaliwa na CAF kwa michezo ya awali wameshauriwa kutumia uwanja wa Azam uliopo Chamazi ambao unakubalika kwenye viwango Shirikisho hilo kwa michezo ya awali.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wakiwemo wa Serikali, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), timu ya Simba, viongozi wa ulinzi na usalama na watoa huduma mbalimbali.

No comments:

Post a Comment