Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Vedastus Mwita (katikati) akizungumza kwenye uzinduzi huo. |
Na Joachim Mushi, Dar
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi
kampeni ya “WALETE,” ikiwa ni sehemu ya kufanya maboresho na kuleta huduma za bora
za mawasiliano ya data na sauti kwa wateja wake.
Kampeni hiyo maalumu itakayojulikana kwa jina la “WALETEE” imelenga
kutoa huduma nafuu za vifurushi vya simu, ikiwa ni pamoja na dakika, Intaneti,
na Ujumbe Mfupi (SMS) vilivyoboreshwa zaidi, kwa ajili ya kuwafaidisha wateja
wa maeneo yote nchi, iwe vijijini ama mjini.
Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la TTCL, Bw. Vedastus
Mwita akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema kuwa
lengo kuu la kampeni ya “WALETE” ni kuwafikia Watanzania wote na kutoa huduma
zinazokidhi mahitaji yao ya mawasiliano, hasa katika nyakati hizi za teknolojia
ya kidijitali.
Amesema kupitia kampeni ya “WALETE,” kumefanyika maboresho
kwa kuongeza BONUS kubwa kwenye vifurushi vya mawasiliano, ikiwemo Dakika, SMS,
na Kifurushi cha Jiachie Xtraa, ambacho kinampa mteja fursa ya kupata muda wa
kutosha wa kupiga simu kwenda mitandao yote na ujumbe mfupi kwa gharama nafuu
na bila ukomo wa muda.
Akifafanua zaidi alisema kifurushi kingine kipya ni ‘T-Connect
Plus’, ambacho kimeongezea muda wa maongezi, ambapo mteja atanunua kifurushi
hicho na kupata faida ya Intaneti, ujumbe mfupi (SMS), pamoja na muda wa
maongezi kwenda mitandao yote.
Aidha ameongeza kuwa kutokana na kukua kwa matumizi ya
kidijitali, wameboresha upatikanaji wa vocha kwa njia ya kidijitali hivyo, kwa sasa
mteja anaweza kupata vocha kupitia mawakala wa T-RUSHA.
“…Vocha zetu kwa sasa pia zinapatikana kwa njia ya
kidijitali kupitia T-Pesa, kwenye Benki ya CRDB, NMB, Selcom, na mitandao
mingine ya simu. Vilevile, vocha za kukwangua bado zinapatikana kwa mawakala
waliopo maeneo mbalimbali na kwenye maduka yetu na vituo vya huduma kwa wateja”
alisema.
Akizungumzia kuhusu kifurushi cha Bufee Tena, ambacho
kimeboreshwa zaidi na kwa gharama nafuu, Mwita amesema kifurushi hicho kinampa
mteja uhuru wa kuchagua kiwango anachotaka, iwe Dakika, SMS, au Data, kulingana
na mahitaji yake.
Naye, Balozi wa kampeni ya “WALETE,” Clayton Chipando
maarufu kama ‘Baba Levo’, ambaye ni mtangazaji maarufu wa kituo cha Wasafi FM
na mwanamuziki, amesema bado anaikubali TTCL kwenye upande wa Intaneti kwani
bado huduma zake ni bora zaidi tofauti na mitandao mingine.
“Mtandao wa TTCL kwenye upande wa Intaneti hapo ndipo
tutakapoonyeshana ukubwa, kwani ndio wapo bora zaidi kwenye kumfanya Mtanzania
kuperuzi kwa haraka zaidi,” alisema Baba Levo na kuwaomba Watanzania warudi
kuutumia mtandao huo kufurahia vifurushi nafuu vya sauti pamoja na Data.
No comments:
Post a Comment