MBARAWA: SIKU ZAHESABIKA KWA WASIMAMIZI WA MIZANI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 20 November 2021

MBARAWA: SIKU ZAHESABIKA KWA WASIMAMIZI WA MIZANI

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa uongozi na wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) (hawapo pichani), katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya uongozi na wafanyakazi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), katika kikao kazi chao jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka wasimamizi na wafanyakazi wa mizani nchini kujitafakari kuhusu mienendo yao ya utendaji kazi kabla hatua stahiki hazijachukuliwa. 

Ametoa angalizo hilo Novemba 19, 2021 jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na uongozi na wafanyakazi wa makao makuu ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na kueleza kuwa pamoja na kufungwa mifumo ya kamera za CCTV bado kumekuwa na malalamiko ya vitendo vya rushwa kwa watumishi katika mizani zilizoko maeneo mbalimbali nchini.

 

"Ni aibu na ni jambo la hovyo mtumishi wa mizani anaenda kuchukua rushwa hadharani na hajali uharibifu unaoendelea wa barabara zetu, huu ni mtandao unaoendelea kuanzia wa chini hadi wa juu, nawaambia na kuwatahadharisha kuwa siku zenu zinahesabika na nitawatoa siku za karibuni," amesema Prof. Mbarawa. 

 

Waziri Prof. Mbarawa amewataka TANROADS kutoa elimu ya kutosha kwa wasafirishaji wote nchini ili kuwasaidia kufahamu haki na wajibu wao katika kusaidia kulinda miundombinu ya barabara na kupunguza malalamiko ya mara kwa mara. 

 

Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka Mtendaji Mkuu wa TANROADS kuhakikisha barabara kuu zinazounganisha mikoa yote nchini zinawekwa vivuko vya waenda kwa miguu au madaraja ya juu pahala panapostahili ili kupunguza idadi ya vifo vya watumiaji wa barabara. 

 

"Tukumbuke kuwa tunajenga barabara si kwa ajili ya magari tu bali na watembea kwa miguu kama moja ya watumiaji wa barabara hizi, Nalisema hili kwa kuwa nimekuwa nikipokea malalamiko kadhaa hasa barabara ya Kimara - Kibaha nendeni mkaweke vivuko", amesisitiza Prof. Mbarawa. 

 

Awali akitoa taarifa ya Wakala, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatius Mativila, amemueleza Waziri huyo kuwa katika mwaka huu wa fedha 2021/22 imejipanga kutekeleza miradi yote ya kimkakati kwa wakati na ubora unaotakiwa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 897.656 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shilingi Bilioni 567.342 zitatumika katika matengenezo ya kawaida, matengenezo ya muda maalum, matengenezo sehemu korofi na matengenezo ya madaraja.

 

Ametaja miradi iliyopangwa kutekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi mpya wa barabara kuu kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 467.11 na barabara za mikoa zenye urefu wa kilometa 103.

 

Eng. Mativila ameongeza kuwa kwa upande wa madaraja, TANROADS itajenga na kukarabati madaraja 21 yaliyopo katika barabara kuu na ujenzi wa madaraja na makalvati makubwa 66 katika barabara za mikoa. 

 

Waziri Prof. Mbarawa anaendelea na ziara yake jijini Dar es Salaam yenye lengo la kukagua miradi inayoendelea kutekelezwa pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi


No comments:

Post a Comment