Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) Taifa, Bi. Martha Makala akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam. |
MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wameitaka Serikali kupitia wizara husika kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 na mapitio yake, na kuweka vifungu vya sheria vinavyopiga marufuku matumizi ya viboko shuleni na adhabu nyinginezo zinazoathiri haki ya kuishi ustawi, na utu wa mtoto.
Ili kuimarisha mfumo wa ulinzi na usalama wa wanafunzi na kuondoa mianya ya matumizi mabaya ya mamlaka na nguvu dhidi ya wanafunzi, hatua ambayo itasaidia kuzuia vitendo vya ukatili ndani na nje ya shule.
TEN/MET na LHRC wamesema hayo leo jijini Dar es Salaam walipokuwa wakizungumza na vyombo vya habari kupinga tukio lililotokea wilayani Busega, Mkoa wa Simiyu, ambapo mwanafunzi Mhoja Maduhu anayesoma kidato cha pili Shule ya Sekondari Mwasamba anadaiwa kufariki dunia baada ya kuadhibiwa kwa kuchapwa viboko sehemu mbalimbali za mwili wake na mmoja wa walimu kwa kosa la kutofanya kazi ya kikundi darasani.
Akifafanua kwa wanahabari, Mratibu wa TEN/MET Taifa, Bi. Martha Makala amesema taasisi yake na LHRC kupitia afua mbalimbali za kupinga ukatili wa kijinsia mashuleni, wamekuwa wakihamasisha jamii na walimu kuhusu matumizi ya mbinu mbadala za kudhibiti nidhamu ya wanafunzi bila kutumia viboko na adhabu kali, kwa kutumia majukwaa ya uchechemuzi na vikao vya kisekta kujadili na kuomba mabadiliko ya sheria na miongozo ili kuboresha ulinzi na usalama wa wanafunzi wakiwa shuleni na nje ya shule.
Alisema takwimu zinaonesha kwa kipindi kifupi cha Januari hadi Februari 2025 huduma ya simu ya kitaifa kwa watoto (116) inayoratibiwa na C-SEMA ilipokea jumla ya kesi 169. Kesi 52 zilikuwa za ukatili na unyanyasaji wa kimwili dhidi ya watoto, kati ya kesi hizo 52 wasichana kesi 21, huku wavulana kesi 31, Aina za ukatili zilizoripotiwa ni kupigwa, kung’atwa, kuchomwa moto sehemu mbalimbali za mwili na adhabu kali ya viboko. Kila siku huduma ya simu ya kitaifa kwa watoto hupokea zaidi ya mawasiliano 10,000 kutoka kwa watoto na jamii.
"...Kwa takwimu hizi ni dhahiri kwamba matukio ya watoto, wanafunzi kufanyiwa vitendo vya ukatili unyanyasaji na ukatili wa jinsia hususani kupewa adhabu kali ya viboko ni nyingi sana katika jamii yetu, ni ukweli usiopingika kwamba suala hili halina manufaa na linapaswa kukomeshwa." Alisema Mratibu huyo wa Taifa wa Mtandao wa wa Elimu Tanzania.
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) Taifa, Bi. Martha Makala akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam. |
Aidha, kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji-LHRC, Wakili, Fulgence Massawe ameiomba Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia kutoa waraka rasmi (circular) unaoelekeza walimu wote kuacha matumizi ya adhabu za viboko na kuelekeza mbinu mbadala za nidhamu zinazolinda utu na haki za watoto, wakati mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Elimu ukiendelea.
Ameongeza kuwa ipo haja ya Serikali kuendelea kuimarisha utekelezaji wa kuanzishwa Madawati ya Ulinzi na usalama kwenye shule zote ifikapo mwaka 2029, huku madawati hayo yakitoa mfumo rasmi wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya watoto wanaokumbwa na ukatili wa aina mbalimbali shuleni.
"...Serikali iwekeze katika adhabu mbadala zisizotweza utu wala kutishia maslahi ya watoto na wanafunzi kwa ujumla, pamoja na kufuatilia pia adhabu zingine ambazo sio za viboko lakini ni mbaya na zinatweza utu wa watoto na kuwasababishia maumivu ya muda mrefu ya kimwili na kiakili, kwani adhabu za viboko zimekuwa zikitajwa kuchangia ongezeko la utoro shuleni, hivyo serikali ikomeshe adhabu hii ili kuhakikisha wanafunzi wanabaki shuleni, wanandelea na masomo na kukamilisha mzunguko wao wa Elimu katika ngazi husika bila vitisho vyovyote," alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji-LHRC, Wakili, Massawe.
Pamoja na hayo ameshauri hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na tukio la kikatili na matukio mengine yanayofanana na hilo ambayo yamevunja haki ya msingi ya mtoto ya kuishi, kinyume na Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Serikali iendelee pia kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa waathiriwa wa ukatili mashuleni na kwamba wahusika wanawajibishwa ipasavyo ili kutoa ujumbe wa wazi kuwa ukatili dhidi ya watoto na wanafunzi wote hautavumilika na haukubaliki.
Tarehe 26 Februari 2025 ziliripotiwa taarifa kupitia vyombo vya habari za kufariki kwa mwanafunzi aitwaye Mhoja Maduhu wa kidato cha pili aliyekuwa akisoma shule ya sekondari Mwasamba iliyopo wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu. Mhoja anadaiwa kufariki dunia baada ya kuadhibiwa kwa kuchapwa viboko sehemu mbalimbali za mwili wake na mwalimu aitwaye kupita kiwango kwa kosa la kutofanya kazi ya kikundi darasani.
No comments:
Post a Comment