WANANCHI MKOA WA MARA WATAKIWA KUTUMIA KWA USAHIHI MIKOPO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 11 March 2025

WANANCHI MKOA WA MARA WATAKIWA KUTUMIA KWA USAHIHI MIKOPO

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw. Gerald Kusaya, akizungumza kuhusu changamoto za mikopo umiza wakati alipokutana na Timu ya Wataalam ya Wizara ya Fedha ambao walifika ofisini kujitambulisha kwa lengo la zoezi la kutoa elimu ya fedha katika mkoani huo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bw. Gerald Kusaya, akiagana na Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Salim Khalfan Kimaro, baada ya Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kufika ofisini kwake kujitambulisha kwa lengo la kuanza kutoa elimu ya fedha mkoani humo.



Na. Peter Haule na Josephine Majura, WF, Mara

KATIBU Tawala Mkoa wa Mara Gerald Kusaya amewataka wananchi wa mkoa huo kutumia mikopo inayotolewa na Serikali kwa manufaa na kuirejesha kwa wakati ili iweze kuwanufaisha wengine wenye uhitaji.
 
Rai hiyo imetolewa Mkoani Mara, alipokutana na kufanya mazungumzo na Timu ya Wataalamu ya Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha ambayo imewasili mkoani hapo kwa ajili ya kutoa elimu katika baadhi ya vijiji vya Wilaya za Mkoa huo.
 
Alisema kuwa uelimishaji umma kuhusu masuala ya huduma za fedha ni jambo la msingi kwa kuwa linatoa fursa kwa wananchi kuweza kufahamu ni namna gani wanaweza kunufaika na mikopo wanayoipata kutoka Serikalini na Taasisi nyingine zinazotoa huduma za Fedha.
 
“Uzoefu unaonesha kuwa wakati mwingine mwananchi anakuwa na shida lakini pale anapodhani anapata fedha za kujikwamua anajikuta amejiingiza kwenye shimo lingine na kuzalisha matatizo makubwa kwake binafsi, familia na jamii inayomzunguka kwa kukosa uelewa”, alieleza Bw. Kusaya.
 
Bw. Kusaya alisema kuwa Serikali imekuwa na mpango mahususi wa kutoa mikopo kwenye vikundi kupitia Halmashauri, lakini utafiti unaonesha kuwa pamoja na jitihada za Serikali kuna watu hawajanufaika na mikopo hiyo kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya mikopo.
 
Aliwataka wananchi wa mkoa huo kutambua kuwa mikopo inayotolewa na Serikali haitolewi kwa maana ya zawadi bali inatolewa kwa kusudi la kumwinua mwananchi kwa suala la kipato na inatakiwa irudishwe ili wengine waweze kunufaika pia.
 
Kwa upande mwingine Bw. Kusaya alishangazwa na tabia za wananchi kukopa kwenye taasisi za “mikononi” ambazo hazina ofisi, ambazo ni dhahiri kuwa ufuatiliaji wa marejesho hauwezi kuwa na ustaarabu, alisema taasisi ya ukopeshaji ni lazima iwe na ofisi, anuani na usajili.
 
Alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wakiwemo wa Halmashauri za Wilaya na Mkoa wakiwa na wasiwasi kuhusu taasisi za ukopeshaji kwa kuwa viongozi hao wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na milango ipo wazi.
 
Bw. Kusaya aliwataka wananchi wa mkoa wa Mara, kuhudhuria kwenye mafunzo ya elimu ya fedha katika kipindi ambacho timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha itakuwa Mkoani humo kwa kuwa mafunzo yatatolewa bila gharama.
 
Alisema utoaji wa elimu ya fedha hususani kwa Mkoa wa Mara ni faraja kwa kuwa wananchi wanaweza kuelimishwa zaidi kuhusiana na matumizi mazuri ya fedha na kujinasua mikononi mwa matapeli wanaotoa mikopo inayotambulika kama kausha damu.
 
Awali Kiongozi wa Timu ya wataalamu wa utoaji wa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Salim Kimaro, alisema kuwa, watu wengi wanakabiliwa na matatizo yanayohusiana na masuala ya fedha yanayowasababishia hasara kubwa kutokana na kukosa elimu ya fedha.
 
Alisema Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini, wametakiwa kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2025/2026 asilimia 85 ya wananchi iwe imefikiwa na elimu hiyo.
 
Alisema Serikali imeandaa Programu ya Kutoa Elimu ya Fedha kwa Umma ya Mwaka 2021/22-2025/26 ikiwa ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21 hadi 2029/30. 
 
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika Sekta ya Fedha imeandaa Nyenzo ya Kufundishia Elimu ya Fedha ambayo imeainisha maeneo muhimu ya kuzingatia wakati wa utoaji wa elimu ya fedha kwa umma ikiwa ni pamoja na usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo, uwekezaji, bima, bima ya amana, kodi na kujipanga kwa Maisha ya uzeeni.

No comments:

Post a Comment