WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameendelea na juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU), katika ziara yake ya kikazi inayoendelea mjini Brussels, Ubelgiji.
Akifanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na viongozi mbalimbali wa EU Aprili 15, 2025, Waziri Kombo amesisitiza dhamira ya Serikali ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania ya kukuza ushirikiano kiuchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, kilimo, utalii, viwanda, utunzaji mazingira, ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, teknolojia, uchumi wa buluu na kuimarisha utendaji wa sekta binafsi.
Waziri Kombo akielezea kuhusu fursa za kiuchumi zinazopatikana nchini kwa viongozi wakuu wa Umoja huo amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mazingira rafiki ya wawekezaji na biashara kupitia maboresho ya sera na sheria, hatua inayolenga kuvutia mitaji ya kigeni na kukuza uchumi wa taifa.
Miongoni mwa Viongozi wakuu wa Umoja huo waliofanya mazungumzo na Waziri Kombo Aprili 15, 2025 ni pamoja na Rais wa Bodi ya Wakurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje, anayesimamia masuala ya Ulaya, na Ushirikiano wa Maendeleo ya Ufalme wa Ubelgiji Bi. Theodora Gentzis, Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya na Mwakilishi wa Juu wa Masuala ya Kigeni na Usalama, Mhe. Kaja Kallas, Makamu wa Rais wa Bunge la UE Mhe. Younous Omarjee, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa UE, Bw. Koen Doens.
Viongozi hao mbali na kuunga mkono wito wa Waziri Kombo wamepongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi huku wakiahidi kuongeza ushikiriano kwa serikali ili kuhakikisha inafikia adhima yake ya kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wake.
Ziara hiyo ya Waziri Kombo, vilevile inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kisiasa kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya wakiwa ni miongoni mwa washirika wakubwa wa kibiashara.
No comments:
Post a Comment