Na Mwandishi Wetu, Chemba
HATIMAYE kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kadri siku zinavyoyoyoma, ndivyo zinavyozidi kunoga na kuchangamka kiasi cha baadhi ya wagombea kwenda kuzisaka kura kwa Mama Lishe na vijiwe vya kahawa.
Mgombea Ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia chama hicho, Halima Okash ambaye aliambatana na Katibu wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Dodoma, Sophia Kiwanga pamoja na baadhi ya viongozi wa CCM Wilaya ya Chemba, amesema baada ya kumaliza vikao vya ndani hawakutaka kupoteza muda waliamua kwenda kuzisaka kura kwa Mama Lishe pamoja na kwenye vijiwe vya kahawa katika mitaa mbalimbali ya Jimbo la Chemba.
Amesema kuwa pamoja na kumuombea kura Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli, lakini vilevile waliunga mkono biashara zao kwa kununua vyakula na kunywa kahawa huku wakimwaga sera pamoja na kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na mgombea huyo.
Okash anasema walipita katika Kata mbalimbali za Chemba ikiwemo Kata ya Msaada, ambapo walikutana na watu wa kada tofauti, wakiwemo wazee, vijana, wanawake, Mama Lishe na wauza kahawa. Anasema wengi wa waliowatembelea na kuwaeleza mafanikio ya Serikali ya CCM inayoongozwa na Dk. Magufuli, walifurahi kuwaona viongozi hao na kwamba walifarijika kwa kuthaminiwa, hivyo kuahidi kumpigia kura Dk Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Kwa kitendo hiki anasema hata wao walifarijika sana kukutana na kada hizo, ambao licha ya kuwaeleza mafanikio aliyoyafanya Dk. Magufuli, lakini hata wao walielezea na kutaja baadhi ya miradi mikubwa inayofanyika katika uongozi wake, ikiwemo; ujenzi wa barabara ya lami ya Dodoma-Manyara, kuunganishiwa umeme kwa gharama ya 27,000, ujenzi wa Reli ya kisasa ya Dar- Dodoma, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma.
Okash, anasema wengi wao wameamini kwamba endapo kwa kipindi kifupi cha uongozi wake Dk Magufuli amefanya mambo yote hayo ya kimaendeleo, basi wakimpa kura na kuchaguliwa tena atafanya maajabu zaidi katika nchi hii.
No comments:
Post a Comment