- THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 6 August 2020

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, akimkabidhi vifaa vya umwagiliaji maji, Mkulima Abdalla Miraji Abdalla mshindi wa Pili wa katika upande wa wajasiriamali wadogo wadogo walioshiriki katika maonyesho ya siku ya Chakula Duniani, huko Chamanangwe Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Na Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuweka kipaumbele katika kufanya tafiti zinazohusiana na sekta za Wizara hiyo kwa kuzingatia mazingira halisi na mahitaji ya wananchi, sambamba na mtukio mbali mbali ikiwemo miripuko ya maradhi ya mazao na mifugo.


Dk. Shein ametowa wito huo leo katika Ufunguzi wa maonesho ya nane nane Chamanangwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Amesema kupitia tafiti hizo, Wizara itaweza kupata taaluma na utaalamu mpya na hivyo kuwafundisha wakulima, akibainisha kuwepo masuala kadhaa yanayohitaji kufanyiwa tafiti.


Akitolea mfano, Dk. Shein alisema yanapotokea maradhi ya mifugo au mazao, Wizara hiyo haipaswi kuishia kupiga dawa pekee, bali inatakiwa kuwa mstari  wa mbele katika kutafuta chanzo cha maradhi hayo, kubuni njia za kuyaondoa pamoja na kuonesha njia ili yasiweze kutokea tena.


Alisema katika siku za hivi karibuni, wakulima wengi wamejikita katika kilimo cha mazao mbali mbali ya biashara ikiwemo Matikitiki, tungule,matango na viazi, kupitia matumizi ya mbolea za kemikali.


Alisema pamoja na uzuri wa kuendeleza kilimo hicho, ipo haja ya kufanya uchunguzi wa kitaalamu juu ya faida na hasara za kilimo cha aina hiyo, hasa katika afya ya udongo, ardhi, mazingira pamoja na virutubishi katika mazao yanayotokana na kilimo hicho.


Aidha,  alisema tangu asili kisiwa cha Pemba kinasifika kwa kuwa na ardhi yenye rutuba nzuri, jambo lilolopelekea kupatikana mavuno mazuri kupitia matumizi ya mbolea za asili (kilimo hai), hali ambayo hivi sasa imebadilika.


“Mimi naamini kilimo hai kwa kutumia mbolea za asili bado kina umuhimu mkubwa ndani ya jamii yetu, hata hivyo suala la kukiendeleza na upatikanaji wa masoko ya mazao yanayotokana na kilimo hicho linahitaji kufanyiwa utafiti”, alisema.


Alieleza kuwa watu wengi duniani wanaendelea kula vyakula vinavyotokana na kilimo hai kutokana na ladha ya asili ya vyakula hivyo pamoja na kuwepo uwezekano wa kupungua athari za kemikali.


Rais Dk. Shein alisema suala la utafiti huzijengea jina taasisi pamoja na nchi katika medani za kitaalamu duniani,kwa kuzingatia mazao yatokanayo na kilimo hai huuzwa kwa bei ya juu sana, ikilinganishwa na mazao yanayotumia mbolea za kemikali.


Aidha, alisistiza umuhimu wa Wizara hiyo kuwahamasisha wananchi juu ya uanzishaji wa mashamba ya viungo (spice farm), ikiwa ni hatua ya kuvutia watalii pamoja na kuwapatia wananchi kipato cha kuendesha maisha yao.


Alisema mashamba hayo yanaweza kuwa sehemu za huduma za vyakula vinavyotumia viungo hivyo, ambapo wageni wataweza kuona uhalisia wa matumizi yake.


“Mnaweza kuwahamasisha wananchi kuanzisha sehemu za maonesho ya wanyama wetu wa asili zitakazokuwa vivutio muhimu kwa wazee na watoto hasa siku za sikukuu, kuna baadhi ya wanyama kama kima na tumbili wanaweza kuwa kivutio kikubwa kwa watalii na wananchi”, alisema.


Katika hatua nyengine, Dk. Shein alisema hatua ya serikali kuanzisha maonesho katika maeneo ya Dole kwa Unguja na Chamanangwe kwa Pemba inatoa fursa kwa wananchi kutambua shughuli zinazofanywa na taasisi zinazoshiriki, ikiwa njia mojawapo ya kujitangaza na kupata masoko.


Alisema pamoja na wananchi kutambua umuhimu wa kufanyika maonesho hayo , idadi kubwa ya washiriki katika hafla hiyo ni uthibitisho wa kuunga mkono na kuthamini juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta za Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, kupitia mipango mikuu ya Maendeleo ya Zanzibar n Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi mkuu wa CCM (2015-2020), ambayo imefikiwa kwa asilimia 95.


Alisema serikali imejipangia mikakati maalum kwa lengo la kuongeza uzalishaji  kupitia mbinu bora, teknolojia ya kisasa, ujenzi wa miundombinu, utoaji wa thamani na upatikanaji wa masoko, pamoja na mitaji na uhifadhi wa chakula, ili kuongeza tija, kukuza uchumi na kuondoa umasikini.


Vile vile alieleza kuwa hatua hiyo imeifanya Serikali kuongeza bajeti ya kilimo , ambapo katika mwaka 2020/2021 imeongezwa kutoka shilingi Bilioni 88.17 (2019) hadi  shilingi Bilioni 129.86 (2020), ikiwa sawa na asilimia 47.3.


Aidha, alisema hatua hiyo imeiwezesha Serikali kutekeleza kwa mafanikio uwamuzi wa kutoa ruzuku ya asilimia 75 kwa ajili ya pembejeo za kilimo na huduma za matrekta kwa wakulima wa mpunga, jambo lililopelekea ongezeko la mavuno ya mpunga kutoka tani 21,014 (2010) hadi tani 47,507 mwaka 2019, kati yake tani 28,734.6 za mpunga zikivunwa kisiwani Pemba.


Dk. shein alisema mazao mengine ya chakula, matunda na mbogamboga nayo yaliongezeka kutoka tani 289,481 (2010) hadi tani 404,285 mwaka 2020, akibainisha zao la muhogo kuvunwa tani 137,692.7, huku tani 65,321.2 za ndizi zikivunwa ambapo kisiwa cha Pemba zilivunwa tani 23,970.5


Akigusia kilimo cha umwagiliaji maji, alisema juhudi zilifanyika kuendeleza kilimo hicho kwa kuendleeza mradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde ya Cheju, Kibokwa na Kilombero (unguja) na Mlemele na Makwarara kwa Pemba katika eneo la hekta 2,200.


Aidha alisema juhudi za kuiendeleza sekta ya Uvuvi zimefanyika, ikiwemo kuifufua Kampuni ya Uvuvi ya Zanzibar (ZAFICO) kwa ununuzi wa Boti mbili, ambapo tayari moja imefika nchini na nyengine inatarajiwa kuwasili mwezi ujao.


Alisema pamoja na hatua hizo Serikali inaendelea na ujenzi wa soko la samaki, mtambo wa kusarifu samaki na chelezo katika eneo la Malindi, ambapo mradi huo utakapokamilika  utaongreza upatikanji wa samaki, kuanzisha viwanda vya usindikizaji, kukuza ajira  na kukuza uchumi wa Taifa.


“Juhudi hizi zimewezesha kuongezeka kiwango cha samaki wanaovuliwa kutoka tani 25,396 (2010) hadi kufikia tani 36,728 mwaka 2019”, alisema.


Kuhusiana na sekta ya Mifugo, Dk. Shein alisema juhudi zimefanywa kuimarisha shughuli za ufugaji, ikiiwemo kuwapatia taaluma wafugaji, huduma za chanjo kwa mifugo ili kuwakinga wanyama dhidi ya maradhi.


Aidha, alisema wananachi wamehamasishwa kaunzisha vikundi vya ufugaji na kupatiwa bure ng’ombe 368 wa maziwa na mbuzi wa maziwa 720 ili kuendeleza ufugaji.


Dk. Shein alisema Serikali iko katika hatua za mwisho za makubaliano ya kuanzisha mradi wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusarifu mwani katika eneo la Chamanangwe kwa kushirikiana na kampuni ya “Ocean Fresh na Kapa Carageenan Nasuntara ya Indonesia”.


Alisema hatua hiyo itachochea kwa kiasi kikubwa ongezeko la bei ya mwani na hivyo kunufaika na kilimo hicho, akibainisha jitihada hizo zimewezesha bei ay zao hilo aina ya Kotoni kuoongezeka hadi shilingi 1,800 kutoka shilingi 800 kwa kilo moja.


Katika hatua nyengie Rais Dk. Shein aliwasihi wanachi kuacha kuchoma moto kwenye maeneo ya kilimo kwani moto huo umekuwa ukiathiri rutuba katika ardhi pamoja na kuua viumbe ambavyo ni muhimu  katika uhai wa  mimea na mazingira.


Aidha, alisiistiza umuhimu wa wananchi kuitunza, kuilinda  na kuiendeleza amani iliopo na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababaisha uvunjifu wa amani.


“Natumia fursa hii kuwaasa vijana kuepuka kuingia katika mtego huo kwa kuhatarisha amani pamoja na maisha yao”, a;isema.


Katika hafla hiyo Dk. Shein alipata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya maonesho, yawemo ya Idara ya Uvuvi, Idara Klimo na wajaasiriamali na kupata maeleo juu ya shughuli mbali mbali zinaofanyika.


Mapema, Waziri wa Wizara Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri aliwataka wananchi na vijana kujiajiri wenyewe na kutumia elimu inayotolewa katika maonesho hayo ili kuongeza uzalishaji, akibainisha maonesho hayo ni dira ya kutoa elimu kutoka kwa watalamu kwenda kwa wananchi.


Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliiasili, Mifugo na Utalii Maryam Abdalla Sadalla alisema kauli mbiu ya maonyesho hayo isemayo “Tudumishe amani navutulivu kwa maendeleo ya sekta ya Kilimo nchini’ inakwenda sambamba na mikakati na Ilani ya Uchaguzi wa CCM (2015-2020).


Alisema uamuzi wa Serikali kuanzisha  maonesho hayo kisiwani humo umetowa fursa kwa wananchi kupata elimu juu ya uendelezaji wa kilimo, mifugo na uvuvi.


Alisema maonesho hayo yamewashirikisha washiriki 189 yakiwa ni suala la kitaifa ambapo watendaji kutoka Hlamashauri za Wilaya, pamoja Uongozi wa Wilaya na Mikoa walishiriki kikamilifu katika maandalizi yake. Hayo ni maonesho ya tatu kufanyika kisiwani humo, ambapo yanafanyika yakienda sambamba na siku ya Chakula Duniani.


No comments:

Post a Comment