SERIKALI YASHINDA KESI YA RUFAA YA KUFUTWA KWA KIFUNGU CHA 148 (5) CHA SHERIA YA MWENENDO WA MASHAURI YA JINAI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 6 August 2020

SERIKALI YASHINDA KESI YA RUFAA YA KUFUTWA KWA KIFUNGU CHA 148 (5) CHA SHERIA YA MWENENDO WA MASHAURI YA JINAI

Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Gabriel Malata akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema leo kuhusu uamzi wa Mahakama ya Rufaa ya kufuta uamzi uliotolewa na ya Mahakama Kuu ya Tanzania ya kuhusu kufutwa kwa kifungu cha dhamana kwa makossa makubwa ya Jinai. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali   jijini Dar es Salaam.


SERIKALI imeshinda kesi ya rufaa ya kufutwa kwa kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania inayozuia dhamana kwa makosa makubwa. Kifungu hicho kinazuia dhamana kwa makossa  ya jinai yakiwemo ya utakatishaji fedha haramu, mauaji, uhaini, unyang’anyi wa kutumia silaha na usafirishaji haramu wa binadamu.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Wakili Mkuu wa Serikali Bwana Gabriel Malata, amesema kuwa Mahakama ya Rufaa mnamo tarehe 5 Agosti 2020, imekubaliana na rufaa ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo ilikuwa ikipinga maamuzi ya Mahakama Kuu yaliyotolewa na jopo la majaji watatu kwa kutamka ya kuwa kifungu cha 148 (5) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kinakinzana na matakwa ya Sura ya 13 (6) (b) na 15 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa.


Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu katika kesi namba 29 ya 2019 iliyofunguliwa na wakili wa kujitegemea Bwana Dickson Paulo Sanga dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika kesi hiyo Bwana Sanga alitaka Mahakama Kuu kufuta kifungu cha 148 (5) kwa kuwa kinakinzana na Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania ambapo mahakama Kuu iliridhia maombi yake.


“Katika rufaa iliyokatwa na Serikali ilipinga maamuzi ya Mahakama Kuu. Mahakama ya Rufaa ambayo iliketi tarehe 6 Julai 2020, pamoja na mambo mengine ilisikiliza hoja za Serikali, kwamba Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania haikinzani na Ibara ya 13 (6) na 15 (1) (2) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Bwana Malata.


“Serikali ilieleza kuwa kifungu hicho cha Sheria kinalenga kutekeleza Ibara ya 13 (3) inayofafanua juu ya misingi ya haki, uhuru na wajibu wa mtu na kwamba haki, uhuru na wajibu unatekelezwa kwa kuzingatia Sheria zingine za nchi na haki, uhuru na haki ya watu wengine”.


Amesema kwa kuzingatia hayo, Mahakama ya Rufaa imefuta hukumu ya Mahakama Kuu na kueleza kuwa Kifungu cha 148 (5) (a) (i), (ii), (iii), (b), (c), (d) na  (e) Sheria ya Mwenendo wa Jinai Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania hakikinzani na Ibara ya 13 (3) na 15(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala yake kinalenga katika kuwezesha utekelezaji mzuri wa Ibara ya 30 (2) inayolenga katika kuhakiksha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi na pia kuhakikisha ulinzi, usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii, afya ya jamii na utekelezaji mzuri wa mipango ya maendeleo ya jamii. 


No comments:

Post a Comment