Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Kheri James (kulia) akivuta pazia kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi la nyumba ya Katibu wa UVCCM wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana. Kutoka kushoto ni Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Alexandrina Katabi, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Manyoni, Lameck Omary na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida Dkt. Denis Nyiraha.
Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Alexandrina Katabi, akizungumza na wajumbe wa umoja huo wilayani Manyoni.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida Dkt. Denis Nyiraha, akizungumza.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Mkoa wa Singida, Yohana Msita, akizungumza na vijana wa umoja huo wilayani Manyoni.
Vijana wa umoja huo wa Wilaya ya Manyoni wakifuatili kikao hicho.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Manyoni, Jumanne Ismail, akizungumza na vijana wa umoja huo wilayani humo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Kheri James (wa nne katikati) akisomewa taarifa ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha VETA kinacho jengwa wilayani Ikungi.
Ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA kinacho jengwa wilayani Ikungi ukiendelea.
Taarifa ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UVCCM wilayani Ikungi ikitolewa kwa Mhe, James.
Vijana wa umoja huo wa Wilaya ya Ikungi wakifuatili kikao hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akizungumza katika kikao hicho.
Wabunge wa Manyoni wakiwa katika kikao hicho. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka na Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahaya Masare.
Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka, akimkabidhi Mhe. James lisiti ya ununuzi wa mabati aliyonunua kusaidia upauaji wa nyumba ya Katibu wa UVCCM wilayani humo.
Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, akizungumza kwenye kikao hicho kuhusu kazi za maendeleo zilizofanya na mgombea Urahis kupitia CCM John Pombe Magufuli.
Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahaya Masare, akizungumza.
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akizungumza.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Kheri James amezitaka Jumuiya za chama hicho kutojihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa mchakato kuelekea uchaguzi mkuu ili kuhakikisha viongozi watakao patikana wanakuwa bora.
James alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wilayani Manyoni na Ikungi wakati akizungumza na viongozi wa CCM pamoja na Jumuiya zake juu ya maandalizi ya uchaguzi katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Singida na ambapo aliwataka kuendelea kupeana ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu, miongozo, kanuni, pamoja na Katiba ya Chama Cha Mapinduzi.
" Kaeni macho na wagombea wanaoibuka katika maeneo yenu wakiomba uwakilishi wa ubunge na udiwani huku wakigawa fedha ili wachaguliwe waulizeni walikuwa wapi siku zote wakati mlipokuwa mnajinyima, mnahangaika usiku na mchana kukijenga chama na iweje waje sasa" alisema James.
Alisema wasikubali kununuliwa na fedha badala yake wachague viongozi bora watakao waletea maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano kupitia chama hicho imara chenye kujali maslahi ya wananchi.
Pamoja na mambo mengine James alikagua utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa UVCCM katika wilaya hizo ambapo katika Wilaya ya Ikungi pia alikagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha VETA na Manyoni aliweka jiwe la msingi la nyumba ya Katibu wa UVCCM.
Wananchi katika wilaya hizo walitoa ahadi mbele yake ya kumpa kura nyingi Mgombea wa nafasi ya Urais John Magufuli, Wabunge na Madiwa kwa asilimia 80 hadi 90.
Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu alisema kura hizo watampa Mgombea huyo kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kuwapelekea miradi mingi ya maendeleo kama vile maji, vituo vya afya, barabara, ujenzi wa madarasa katika shule za msingi na sekondari na Umeme wa REA.
"Kwa kazi hizi alizozifanya mgombea wetu katika jimbo la Singida Magharibi tutampa kura si chini ya asilimia 90" alisema Kingu.
Akizunguzia mchango wake wa ujenzi wa nyumba za makatibu wa UVCCM mkoani hapa alisema nyumba ya Katibu wa Wilaya ya Singida mjini alichangia sh.1,300,000 kwa kununua mabati 60 kwa ajili ya upauaji na kwa nyumba ya Katibu Ikungi ametoa sh.1,800,000 jumla ikiwa ni sh. 3,100,000.
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, alisema kwa kazi kubwa aliyofanya Rais katika jimbo hilo asiwe na wasiwasi atapata kura nyingi kutoka kwa wananchi.
Alisema Rais Magufuli katika jimbo hilo ambalo lilikosa mwakilishi mzuri hapo awali amewapelekea visima vya maji 15, amewapatia sh,bilioni 2 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji na pia amewajengea barabara.
"Ikiwa hiyo haitoshi RaisMagufuli ametupatia sh.bilioni 1.5 kwa aliji ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya na sh.bilioni 2 za ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA" alisema Mtaturu.
Alisema uchaguzi wa mwaka 2015 licha ya kuwepo upinzani mkubwa alipata asilimia 62 ya kura zote sembuse sasa ambapo amefanya kazi hiyo kubwa aondoe wasiwasi ategemee ushindi mnono.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo alisema katika wilaya hiyo amefika kata zote na kati ya vijiji 101 zaidi ya vijiji 68 amevitembelea na kuwa ushindi wa CCM upo wazi kwani wananchi na Wana CCM wanakipenda chama chao na Rais Magufuli.
"Ni ukweli usiopingika Rais Magufuli katika wilaya yetu anatuletea zaidi ya sh.bilioni 400 kwa ajili ya Halmashauri, mishahara na shughuli mbalimbali za maendeleo ambayo yanaonekana na nimefika katika majimbo ya wabunge wetu hawa wawili Elibariki Kingu na Miraji Mtaturu na kulala huko wananchi wanawaongelea vizuri na nimefanya semina na viongozi wote sifa za ushindi wanazo," alisema Mpogolo.
Alitaja sifa ya kwanza kuwa ni kujiandikisha katika daftari la mpiga kura, sifa ya pili ni umoja uliopo kati ya serikali na chama pamoja na wananchi na sifa ya tatu ni wagombea wa chama hicho watasemwaje lakini mgombea wa chama chetu Rais Magufuli anasemwa vizuri sana na watamchagua kutokana na kuwa na imani naye na hao wagombea wengine.
Alisema katika mchakato wa uchaguzi mkuu yeye kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama hata kubali kuona ulaghai na njama zozote za kuhujumu kura za wagombea hao.
Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka alisema katika jimbo hilo wamejipanga vizuri kwenye shughuli za kuinua uchumi ambapo kundi la vijana ndiyo tegemeo lao.
Alisema hivi sasa Manyoni Mashariki wameanzisha kilimo cha korosho na wamepanda ekari 16,000 na kuwa kufikia 2020-2025 watakuwa wamepanda ekari 30,000 ambapo wanatarajia kupata sh.bilioni 80 kwa mauzo ya korosho.
Mtuka alitumia mkutano huo kutoa mchango wake wa kupaua nyumba ya Katibu wa UVCCM wilayani hapo ambapo tayari mabati yote amekwisha yanunua.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti huyo wa UVCCM Taifa aliongozwa na Mwenyeji wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida Dkt. Denis Nyiraha, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa,Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa Pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Siasa na Utekelezaji Mkoa ambapo leo atamaliza ziara yake kwa kutembea Wilaya ya Singida mjini na Singida Vijijini.
No comments:
Post a Comment