WALIOAMBUKIZWA CORONA NCHINI KENYA WAFIKIA 1,618 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 29 May 2020

WALIOAMBUKIZWA CORONA NCHINI KENYA WAFIKIA 1,618



Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe.

KENYA imeripoti maambukizi zaidi mapya 147 na kufikisha idadi ya walioambukizwa hadi 1,618.

Wagonjwa wote 147 waliothibitishwa kuambikizwa ni raia wa Kenya na mdogo zaidi akiwa na umri wa mwaka mmoja, kwa mujibu wa Bwana Kagwe.

Aidha idadi ya waliokufa pia nayo imeongezeka kwa watu watatu zaidi na kufikisha jumla ya watu 58.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema katika mkutano kuwa wagonjwa 13 wa virusi vya corona waliruhusiwa kuondoka hospitali hii leo katika kipindi cha saa 24 zilizopita na kufikisha idadi ya waliopoona nchini humo hadi 421.

Idadi ya waliotangazwa hii leo kupata maambukizi ndio kubwa zaidi tangu kutangazwa kwa mgonjwa wa kwanza nchini humo Machi 13.

"Leo, tumethibitisha idadi ya juu zaidi ya walioambukizwa virusi vya corona ya watu 147 kati ya 2,831 waliofanyiwa vipimo. Idadi ya waliopimwa hadi kufikia sasa ni 70,172," Waziri amesema.

Kati ya watu 147 walioambukizwa, 87 ni wanaume huku 60 wakiwa wanawake. Waziri amesema kulingana na takwimu za serikali, wanaume ndio walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya virusi vya corona ikilinganishwa na wanawake.

Wiki iliyopita, Wizara ya Afya nchini humo ilitahadharisha kwamba wananchi wajiandae kwa idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya kila siku na kusisitizia kuwa kilele cha ugonjwa wa Covid-19 kulingana na mwenendo wake kwa sasa hivi kitarajiwe baina ya mwezi Agosti na Septemba.

''Tunatabiri kwamba kilele cha ugonjwa huu kwetu, kitakuwa miezi ya Agosti hadi Septemba ambapo tutakuwa tunarekodi waathirika karibia 200 kwa siku, hilo ni ikiwa tutaendelea na hatua tulizoanza kuzitekeleza hii leo,'' alieleza Mkurugenzi wa Afya ya Umma Patrick Amoth Alhamisi ya wiki iliyopita.

Pia alidokeza kuwa Kenya inapanga kuanza kupima watu zaidi ya 3,000 kwa siku baada ya kupata vifaa vya kutosha vya kupima virusi vya corona ambavyo vinaweza kudumu hata kwa mwezi mzima.

''Kwa kiwango cha upimaji tunacho lenga, tunaona idadi ikiongezeka lakini hili halifai kuwatia wasiwasi...''
-BBC

No comments:

Post a Comment