Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam
WAJUMBE wa Sekretareti ya Baraza la Mawaziri wamefanya ziara katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kujifunza na kupata uelewa kuhusu ufuatiliaji na tathmini ya namna uwanja huo unavyoendeshwa.
Ziara hiyo imefanyika Juni 10, 2023 jijini Dar es Salaam katika uwanja huo ambao ni uwanja wa nyumbani wa timu za Taifa katika michezo mbalimbali ikiwemo Taifa Stars, Serengeti Girls, Twiga stars pamoja na mataifa mengine jirani.
Akiongea na Wajumbe hao Sekretareti ya Baraza la Mawaziri, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amewaarifu kuwa uwanja huo unatumiwa pia na mataifa jirani ikiwemo nchi ya Burundi, Kenya, Sudan Kusini pamoja na Uganda.
Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema kuwa uwanja huo kwa sasa unafanyiwa ukarabati mkubwa ambao utalazimu kufungwa kwa miezi kadhaa katika eneo la kuchezea mpira, eneo la kukimbilia wanariadha, taa za uwanja, viti vya kukaa wachezaji wakati mechi inaendelea, chumba cha waandishi wa habari cha kurushia matangazo, chumba cha mkutano na waandishi wa habari, viti vya watazamaji, ubao wa matokeo, mifumo ya maji, chumba cha kubadilishia nguo wachezaji pamoja na eneo linalotumiwa na wageni mashuhuri ili uwanja huo uendane na viwango vya CAF na FIFA.
Kwa upande wake kiongozi wa msafara wa wajumbe hao ambaye pia ni Karani wa Baraza la Mawaziri Bw. Nsubili Joshua amesema kuwa wamefarijika na wamejifunza mengi kuhusu uwanja huo ikiwemo namna bora ya kuendesha uwanja huo ili kuongeza mapato ya Serikali na kuwapa burudani Watanzania.
Ziara hiyo imehudhuriwa pia na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Bi. Neema Msitha, Kaimu Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa Milinde Mahona pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo.
No comments:
Post a Comment