NA MWANDISHI
WETU
SERIKALI
imeipongeza Benki ya NMB kwa kuzindua Mfuko Maalum uliotengewa Sh. Bilioni 100
za kukopesha wasambazaji na wauzaji wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Watanzania,
na kwamba Serikali itaingia kifua mbele katika Mkutano Mkuu wa Nishati wa Wakuu
wa Nchi za Afrika (Mission 300), unaofanyika Januari 27 na 28 jijini Dar es
Salaam.
Pongezi hizo
zimetolewa na Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko, wakati wa uzinduzi wa mfuko
huo, aliobeba dhamira chanya ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika Mkakati
wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) na kwamba tukio
hilo ni uthibitisho tosha wa ushirikiano uliopo baina ya Serikali na Sekta
Binafsi katika kustawisha jamii ya Watanzania.
Kwa niaba ya
Serikali na Wizara ya Nishati, Dk. Biteko aliishukuru NMB kwa wazo hili na
kwamba wako tayari kuwaunga mkono ili jambo hilo likatimizwe, huku akisema wazo
la kuhakikisha mawakala na wasambazaji wa nishati safi za kupikia wanapata
mitaji ili kufikisha huduma mijini na vijijini, litasaidia kuchochea upatikanaji
na matumizi ya nishati hiyo.
“Hakika
mpango huu wa NMB kutenga Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya jambo hili,
unastahili pongezi kubwa sana, hasa ikizingatiwa kuwa kama benki ina njia
nyingi sana za biashara, ambazo wangeweza kuwekeza fedha hizo sehemu nyingine
ili kuweza kuendelea kujizalishia faida zaidi.
“Lakini,
msukumo huu wa kuja kuweka kiasi hiki kwenye Nishati Safi ya Kupikia inaonesha
dhamira ya dhati ya benki kuchangia maendeleo endelevu kwa taifa letu la
Tanzania, lakini ni kielelezo tosha cha uzalendo wa kweli uliopo kati yenu
Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa benki hii.
“Mtendaji
Mkuu wa NMB tayari ameeleza hapa faida mbalimbali za matumizi ya Nishati Safi
ya Kupikia na mimi nisisitize kuwa, faida hizo za Afya Bora, Mazingira Safi, Kuboresha
Uchumi na Ufanisi wa Nishati hizi na ukweli kuwa nishati safi ni salama, ndio
maana hata Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara wa hili nchini, Afrika na
duniani kote.
“Wote tunafahamu kwamba, licha ya ukosefu wa
mitaji, changamoto kubwa ya wananchi kuendelea kutumia nishati isiyo safi ya
kupikia, ni ukosefu wa elimu juu ya nishati safi ya kupikia, hivyo suala la NMB
kuanza pia kutoa elimu ya hili ni jambo zuri na la kipekee sana kwa ustawi wa
matumizi ya nishati hii safi.” Alisema Dk. Biteko.
Alibainisha
kuiwa shukrani na pongezi kwa NMB hazitaishia tu katika Nishati Safi ya Kupikia
tu, bali zinaenda pia kwa mambo makubwa ambayo imekuwa ikifanya kwa manufaa kwa
taifa letu la Tanzania, ikiwemo misaada mbalimbali mashuleni, zahanati, vituo
vya afya na hospitali na kuchagiza maendeleo endelevu kwa jamii, sambamba na
upandaji miti.
Januari 27
na 28, Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano uliopewa jina la Mission
300 kuakisi dhamira ya kuwafikia watu milioni 300 barani Afrika kuhakikisha
wanatumia Nishati Safi, ambapo zaidi ya marais 25, Mawaziri wa Fedha na Nishati
60 wa Afrika, watashiriki mkutano huo, mweji akiwa Rais Dk. Samia Suluhu
Hassan.
Kwa kutambua
umuhimu wa Mkutano huo na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania
kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, NMB
inaamini kiasi ilichotenga kwa ajili kukopesha wadau wa biashara ya Nishati
Safi, utakuwa na mchango chanya kwa Taifa katika azma yake ya kukuza kiwango
cha matumizi ya nishati hiyo mjini na vijijini.
Awali, Afisa
Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema msukumo wa benki yake kutenga
kiasi hicho kikubwa cha pesa za kukopesha wafanyabiashara na wasambazaji wa
nishati, unalenga kuwezesha utunzaji wa mazingira, kuboresha afya na ustawi wa
jamii, kukuza uchumi na kuchangia kufikiwa kwa Malengo Endelevu ya Umoja wa
Mataifa ya Mwaka 2030.
Akizungumza
katika uzinduzi huo, Bi. Zaipuna alisema lengo ni kuongeza urahisi katika
upatikanaji wa nishati safi kwa Watanzania na kwamba, NMB inatambua umuhimu wa
kuungana na Serikali kufanikisha Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi,
wenye lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu, kwa urahisi, endelevu
na ya kisasa kwa wote.
“Kama
ulivyoainisha katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
(2024-2034), ‘‘Umuhimu wa agenda hii kwa Taifa letu la Tanzania, na dunia nzima
kwa ujumla, unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya
tabianchi, pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo
safi ya kupikia.’’
“Takwimu
zilizotolewa wakati wa Mkutano wa Clean Cooking uliofanyika jijini Paris,
Ufaransa, Mei, 2024, zinaonyesha kwa nini wadau wote tunapaswa kushirikiana na
Serikali, na Wananchi kukabiliana kwa haraka na suala la ukosefu wa upatikanaji wa Nishati Safi ya
kupikia barani Afrika.
“Takwimu
hizo, ambazo ni za kushtusha, zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu Bilioni 1.2
barani Afrika hawatumii Nishati Safi za kupikia, na kuwalazimu kutegemea mkaa
na kuni kwa kupikia, hali inayochangia madhara makubwa ya kiafya, kimazingira
na kijamii na waathirika wakuu wa changamoto hii ni wanawake, ambao ni dada
zetu, na mama zetu, hasa wa vijijini.
“Matokeo
yake, Afrika inapoteza zaidi ya wanawake na watoto 600,000 kila mwaka kutokana
na athari za moshi wa utokanao na nishati chafu, na Tanzania, kama
ilivyoanishwa na Afisa Nishati Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Mussa Abbas,
zaidi wa watu 33,000 hufariki Tanzania kila mwaka kwa athari za Nishati Chafu,”
alisema Bi. Zaipuna.
Alibainisha
kuwa, kiwango cha mwisho kwa mkopaji mmoja ni Sh. Bil. 1, ambao utakuwa wa riba
nafuu na rafiki ya asilimia 1 kwa mwezi
(sawa na asilimia 12 kwa mwaka) na kuwa walengwa wakuu wa mkopo huu
utakaopatikana kwenye matawi yote, ni wasambazaji na mawakala wa mitungi na
majiko ya gesi ambayo kwa sasa ndio nishati safi zaidi inayopatikana kwa
urahisi.
Aidha,
akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu kuzungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba, aliipongeza NMB kuunga mkono juhudi za Serikali
kufanikisha malenpo endelevu ya kufikisha huduma ya nishati kote nchini na
kwamba benki hiyo imefanya jitihada kubwa katika kuwapambania Watanzania,
wakiwemo wafanyabiashara na wajasiriamali wanawake.



No comments:
Post a Comment