Baadhi ya nyavu za uvuvi haramu zikiteketezwa. |
OPERESHENI ya kupambana na uvuvi haramu katika ziwa Tanganyika kanda ya Kasanga, mkoani Rukwa imefanikiwa kukusanya shilingi milioni 90 ndani ya mwezi mmoja ikiwa ni adhabu mbalimbali kwa wavuvi waliokiuka sheria za uvuvi na.22 ya mwaka 2003 pamoja na sheria ya mazingira na.20 ya mwaka 2004.
Hayo yamesemwa na kiongozi wa operesheni hiyo Geofrey Salaka wakati akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo baada ya kutembelea katika soko la samaki la kasanga na kuongea na maafisa wa operesheni hiyo.
Salaka alisema kuwa mbali na kuwatoza faini hizo pia wamefanikiwa kutoa elimu na kuwahamasisha wavuvi wadogowadogo kulipia leseni zao za uvuvi na leseni za vyombo wanavyovitumia kwa shughuli za uvuvi kama sheria inavyotaka huku akielezea changamoto wanazozipata katika kutekeleza majukumu hayo.
“Changamoto tunazozipata ni pamoja na kukumbana na fujo kutoka kwa wananchi utoroshwaji wa samaki na mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi, kuwepo raia wa kigeni wakijihusisha na shughuli za uvuvi, hali ya hewa, upepo mkali, mvua na mawimbi ziwani,” Alisema.
Kwa upande wake Mh. Wangabo alipongeza juhudi hizo za kuhakikisha mapambano dhidi ya uvuvi haramu hayarudi nyuma ili kutunza na kuhifadhi samaki na mazingira katika ukanda wa Ziwa pamoja na Ziwa lenyewe na kusisitiza elimu iendelee kutolewa kwa wavuvi ili washiriki katika kutunza mazingira.
“Tuendelee kuwaelewesha wavuvi, vinginevyo wataendelea kuharibu rasilimali ya taifa letu, na hii ni kwaajili yetu sisi na vizazi vinavyokuja, tukivua katika hali ambayo haina uvuvi endelevu tutawafanya hawa samaki mwishoni watakwisha, wakiisha hawa watu watakwenda wapi, maisha yao yanategemea hapa lakini hawajui hilo, wanataka waharibu mpaka kambi sijui watalala wapi,” Alisema.
Na kuongeza kuwa atahakikisha anafanya mkutano na wananchi na wavuvi hao ili kuweza kuwaelimisha juu ya madhara yanayoweza kujitokeza kama uvuvi haramu utaendelea kutekelezwa bila ya usimamizi wowote.
Operesheni hiyo ilianza tarehe 19.10.2018 na Miongoni mwa zana zilizokamatwa katika operesheni hiyo ni pamoja na Injini za boti 10, mitumbwi 48, magari 9 ya kusafirisha samaki, pikipiki 4 zilizokuwa zinasafirisha samaki, samaki wachanga kilo 2050, nyavu 250 za makila chini ya nchi tatu pamoja na nyavu 20 za timber (monofilament nets).
No comments:
Post a Comment