Na Farida Ramadhani, Dodoma
NAIBU Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande ametoa wito
kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzaber kujenga Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa
kutumia wataalam wa ndani ili kusimamia kikamilifu fedha za Serikali
zinazotumika katika ununuzi.
Alitoa wito huo jijini Dodoma alipokutana na
kufanya mazungumzo na Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar
iliyotembelea Mamlaka ya Ununuzi wa Umma nchini (PPRA) kwa ajili ya kujifunza
masuala ya ununuzi wa umma kwa ujumla.
Alisema Mfumo huo pia utasaidia kurahisisha
mchakato wa ununuzi pamoja na kuongeza uwazi wa zabuni kwa kujua thamani halisi
ya fedha.
Aidha Mhe. Chande aliipongeza Kamati hiyo kwa
kufanya uamuzi wa kuja kujifunza PPRA katika kipindi hiki ili kwenda kuboresha
Muswada wa Sheria ya Ununuzi ambao utajadiliwa katika Baraza la Wawakilishi
Zanzibar.
“Haya ni maamuzi sahihi kwa sababu Taasisi za
Umma ndio ambazo zinatumia bajeti kubwa katika ununzi wa umma kwa kuwa zaidi ya
asilimia 70 ya Bajeti zetu zinakwenda kwenye ununuzi, kwa hiyo tunapoenda
kupitisha Mswada wetu tuhakikishe Sheria imewekwa vizuri ili kuepuka
changamoto”, aliongeza Mhe. Chande.
Aliwakaribisha kutembelea PPRA mara kwa mara kwa
ajili ya kuendelea kujifunza zaidi na ikiwezekana waende jijini Arusha ambako
kumesimikwa Mfumo wa Ununuzi ili waone uhalisia uliopo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti
ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mwanaasha Khamis Juma alisema kwa sasa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya maboresho ya Sheria ya Ununuzi,
hivyo kamati imeamua kuja kujifunza ili waweze kuishauri Serikali kikamilifu.
“Kama nilivyosema hapo awali, hii ni Kamati ya
Bayeti na kazi yeke ni kupitisha Bajeti ya Serikali ambayo ndani yake kuna
miradi na kwenye miradi kuna ununuzi, kwa hiyo tumeamua tuje tuone wenzetu
wanafanyaje, Sheria zao zikoje, ili tuone namna bora ya kuishauri Serikali”,
aliongeza Mhe. Mwanaasha.
Naye Naibu Waziri wa Ofisi ya Raisi, Fedha na
Mipango, Zanzibar, Mhe. Juma Makungu Juma, alisema wamekuja kujifunza kwa
sababu fedha nyingi za Taifa zinatumika katika ununuzi hivyo ni muhimu Serikali
ihakikishe fedha hizo zinatumika vizuri.
Alisema kuwa wamekuja kuchukua uzoefu wa
taratibu mbalimbali za ununuzi pamja na mafanikio kwa sababu taratibu hizo za
zinatofautiana kati ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kujadili mafanikio
na changamoto zilizopo katika masuala ya ununuzi.
.jpg)

No comments:
Post a Comment