Na Prisca Ulomi, WUUM, Dodoma
KATIBU Mkuu mpya wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula, amewasili rasmi leo Wizarani hapo Mji wa Serikali, Mtumba, Dodoma kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Sekta hiyo mara baada ya kuhamishwa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Dkt. Chaula amesema kuwa amefurahi na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumhamishia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili kuwa Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano kwa kuwa anafahamu umuhimu na mchango wa Sekta hiyo katika maeneo mengine kwa kuzingatia kuwa amekuwa akitumia TEHAMA katika kutekeleza majukumu yake alipokuwa TAMISEMI na Wizara ya Afya
“TEHAMA itatutoa kwenye chagamoto, lazima tuwekeze na tuitumie kama fursa, suala sio wingi wa watu, kuwa na watumishi wengi, kwa kuwa mnaweza kuwa wengi ikawa vurugu, ila mnaweza kuwa wachache na mkafanya kazi vizuri, binafsi nimetumia TEHAMA kwenye sekta ya afya na TAMISEMI, nimekuja huku nimefurahi, nitaendelea kujifunza zaidi, nanyi ndio wataalamu, mjiamini, msiwe na hofu, watanzania tuna akili, uwezo tunao,” amesisitiza Dkt. Chaula
Katibu Mstaafu wa Sekta hiyo, Dkt. Maria Sasabo, akizungumza wakati anamkaribisha na kumkabidhi ofisi Dkt. Chaula, Dkt. Sasabo alisema kuwa Sekta ya Mawasiliano ni mtambuka, inategemewa na Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu mbali mbali ya kila siku ambapo tayari kuna Sera, sheria, miongozo na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa Sekta ikiwa ni pamoja na miundombinu ya mawasiliano ambayo inawezesha utendaji kazi wa mifumo ya kielektroniki nchini
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alimweleza Dkt. Chaula kuwa Sekta hii imetekeleza vema majukumu yake katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2019/2020 na sasa wanajiandaa kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwenye Bunge la bajeti linaloendelea mjini Dodoma
Kamwelwe amemwagiza Dkt. Chaula kuhakikisha kuwa Sera ya Taifa ya Posta inahuishwa ili iweze kwenda na wakati kwa kuwa sekta ya posta imebadilika na Shirika la Posta limebadiilisha namna ya kufanya kazi na kuhudumia wananchi kwa kuwa linatumia TEHAMA kutoa huduma na kusafirisha vifurushi na vipeto kwa wateja
Akisalimiana na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashata Nditiye mara alipowasili ofisini kwake kujitambulisha, Nditiye alimwarifu Dkt. Chaula kuwa Sekta ya Mawasiliano ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa taifa letu kwa kuwa sasa ni moja ya Sekta tano bora kwa kuongoza kuchangia pato la taifa na hata Bungeni maswali mengi yanayoulizwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za mawasiliano
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa amemweleza Dkt. Chaula kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano viongozi wanafanya kazi kama timu moja bila kujali anasimamia Sekta ipi na mara nyingine amekuwa akishiriki kazi za Sekta ya Mawasiliano ikiwa ni pamoja na kujibu maswali Bungeni
Akizungumza na Menejimenti na wawakilishi wa taasisi za Sekta hiyo Wizarani hapo, Dkt. Chaula amesema kuwa anategemea kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi na wafanyakazi kwa kuwa kwenye kazi tunatengeneza upendo, marafiki na kuwa ndugu na sio maadui, tunafungua njia. Hivyo, amewataka kufanya kazi vizuri kama uko nyumbani kwako kwa ajili ya wengine
Pia, amewakumbusha kuendelea kuzingatia miongozo na maelekezo ya Wizara ya Afya ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ili kujilinda na maambukizi ya virusi vya Corona ambavyo ni janga la dunia ambapo kwa Tanzania Serikali imejitahidi na kujidhatiti kuhakikisha kuwa maambukizi yanaendelea kupungua na wagonjwa wanapona na amewataka wasiwe na hofu kwa kuwa Corona ni mafua tu
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment