SERIKALI YAPOKEA MSAADA WENYE JUMLA YA SHILINGI BILIONI 14.97 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 28 April 2020

SERIKALI YAPOKEA MSAADA WENYE JUMLA YA SHILINGI BILIONI 14.97

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akipokea msaada wa fedha kutoka taasisi ya Rotary Club Tanzania, ikiwa ni kusaidia mapambano ya ugonjwa wa Corona nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania, Bw. Gabriel Malata akikabidhi Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu msaada wa shilingi milioni 700 ili kusaidia katika mapambano ya COVID-19.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza BAADA ya kupokea msaada wa fedha kutoka Airtel Tanzania, Rotary Club Tanzania na Kampuni ya Bia ya Serengeti.

Mwenyekiti wa Bodi wa Airtel Tanzania, Bw. Gabriel Malata akitangaza msaada wa shilingi milioni 700 kusaidia juhudi za Serikali za kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Na John Stephen, WAMJW – MNH, Dar es Salaam 

SERIKLI imepokea msaada wa shilingi bilioni 14.9 kutoka kwa makampuni ya Airtel Tanzania, Rotary Club Tanzania, Serengeti Breweries na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Kifua Kikuu, UKIMWI na Malaria (Global Fund), ambazo sehemu kubwa zitatumika kununua vifaa kinga kwa watumishi wa afya na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wenye maambukizi ya ugonjwa wa Corona (COVID-19).

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameyasema hayo wakati akipokea msaada wa fedha zenye jumla ya shilingi milioni 950 na lita 1,250 za vitakasa mikono zenye thamani ya shilingi milioni 15 ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa Corona.

Waziri Ummy amefafanua kwamba Global Fund imetoa shilingi bilioni 14, Airtel Tanzania shilingi milioni 700 na Rotary Club Tanzania shilingi milioni 250.

“Tumepokea shilingi bilioni 14 kutoka Global Fund, shilingi bilioni 9.6 tumezitoa kwa ajili ya kununua vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa Afya, lakini pia fedha zilizotolewa na Airtel na Rotary Club Tanzania tutazielekeza huko. Kipaumbele chetu ni kuwalinda watumishi wa afya,” amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

“Natumia fursa hii kuwashukuru watumishi wa afya ambao wamekuwa wakijitoa usiku na mchana katika kutoa huduma kwa watu waliopata maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19) pamoja na wale wahisiwa. Kipaumbele cha Serikali ni kuwalinda watumishi wa Afya kwa kununua vifaa kinga kwani fedha tulizozipata hapa tutazielekeza kwenye ununuzi wa vifaa kinga. Niendelee kuwaisistiza Watumishi wa Afya wazingatie miongozo ya magonjwa ya kuambukiza,” amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Amesema watumishi wa afya ambao wamepatiwa mafunzo katika vituo vya kutoa huduma kwa wathirika wa ugonjwa wa Corona, hakuna aliyepata maambukizi kwa kuwa wanazingatia miongozo ya Serikali ya kutoa matibabu kwa wagonjwa wa Covid-19 pamoja na miongozo ya magonjwa ya kuambukiza.

Waziri amesema ushiriki wa kila mdau katika mapambano dhidi ya maambikizi ya virusi vya Corona ni muhimu na kwamba msaada uliotolewa na kampuni hizo ni mkubwa katika mapambano ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

“Napenda kurudia tena kwa niaba Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, nawashukuru Airtel Tanzania, Serengenti Breweries na Rotary Club kwa hiki mlichotupatia. Asanteni sana,” amesema Waziri Ummy.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Airtel Tanzania, Bw. Gabriel Malata amesema Airtel Tanzania imetoa shilingi milioni 700 ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na janga la Corona.

“Sisi bodi ya wakurugenzi wa Airtel na kwa niaba ya Airtel Tanzania, tunatambua juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Corona, lakini pia tumejitathimini na kutambua kuwa sisi kama Airtel hatuwezi kuendelea bila kuwepo watu wanaotumia huduma zetu. Watu hawa ndio mtaji wa Kampuni,” amesema Bw. Gabriel.

Naye Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Bia ya Serengenti, Bw. John Wanyancha amesema kuwa kampuni hiyo imetoa lita 1,250 ya vitakasa mikono nyenye thamani ya shilingi 15 milioni kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na maambukiza ya virusi.

Mwenyekiti wa Rotary Club, Bi. Agnes Batengas amesema Rotary imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19).

“Shilingi milioni 183 zitatumika kutoa msaada wa vifaa vya kujikinga (PPE), vifaa vya maji safi ambavyo vitasambazwa katika vituo maalumu vya kuhudumia wagonjwa wa Corona jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Amana, Zanzibar, Hospitali ya Mawenzi na Hospitali ya Mount Meru,” amesema Bi. Agnes.

Amesema shilingi milioni 67 zitatumika katika kutekeleza miradi ya kudhibiti ugonjwa wa Corona nchini kupitia Club za Rotary.

No comments:

Post a Comment