SERIKALI KULIPA MIL 315.1 ZA WAKULIMA WA MUZIA AMCOS MKOANI RUKWA – MHE HASUNGA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 15 October 2019

SERIKALI KULIPA MIL 315.1 ZA WAKULIMA WA MUZIA AMCOS MKOANI RUKWA – MHE HASUNGA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na wanachama wa Muzia Amcos ya Wilayani Kalambo katika mkoa wa Rukwa jana tarehe 13 Octoba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Rukwa, Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe Joachim Wangabo na mwingine ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe Julieth Binyura. (Picha Zote Na Mathias Canal).

Sehemu ya wawakilishi wa Wanachama wa Muzia Amcos ya Wilayani Kalambo katika mkoa wa Rukwa wakimsikiliza Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akitatua kadhia za chama hicho kuhusu kutapeliwa fedha na Mwenyekiti wa chama hicho Ndg Linus Kalandamwazye kiasi cha Shilingi Milioni 315.1 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Rukwa.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe Joachim Wangabo na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe Julieth Binyura wakijadili jambo mara baada ya kumalizika kikao kazi kuzungumza na wanachama wa Muzia Amcos ya Wilayani Kalambo katika mkoa wa Rukwa jana tarehe 13 Octoba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Rukwa.


Sehemu ya wawakilishi wa Wanachama wa Muzia Amcos ya Wilayani Kalambo katika mkoa wa Rukwa wakimsikiliza Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akitatua kadhia za chama hicho kuhusu kutapeliwa fedha na Mwenyekiti wa chama hicho Ndg Linus Kalandamwazye kiasi cha Shilingi Milioni 315.1 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Rukwa.


Na Mathias Canal, Rukwa

SERIKALI imetangaza dhamira yake ya kuwalipa wakulima 156 wa mahindi jumla ya Shilingi 315,118,510 kutokana na kuzulumiwa na mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Ndg Linus Kalandamwazye.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ametoa kauli hiyo jana tarehe 13 Octoba 2019 wakati akizungumza na wanachama wa Muzia Amcos Wilayani Kalambo wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Rukwa.

Malipo hayo yatawahusu wakulima wa Tarafa ya Mwimbi yenye kata nne ambazo ni Mambwe Kenya, Ulumi, Mkombo na Mwazye kutokana na kupima mahindi yao zaidi ya Tani 622.679 kwenye Chama cha Muzia Amcos kilichopewa uwakala na serikali wa kununua mazao kwa wakulima tarehe 8 Agosti 2017 kwa makubaliano ya kulipwa ndani ya wiki tatu kutoka tarehe ya kupimwa lakini hawakulipwa mpaka sasa.

“Kesi ikiwa mahakamani serikali haiwezi kuingilia badala yake wakati tunaendelea na kesi hiyo ninaziagiza taasisi zangu tatu kuchanga fedha kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao” Alikaririwa Mhe Hasunga

Alisema wanaotakiwa kuchanga fedha hizo kwanza ni Wizara ya Kilimo kwa kushindwa kulishughulikia jambo hilo kwa wakati ili wakulima hao waweze kulipwa fedha zao.

Ameiagiza pia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuchanga fedha hizo kwani wao ndio wasimamizi wa Vyama vya Ushirika lakini kwa kipindi chote wameshindwa kushughulikia changamoto hiyo ya wakulima.

Kadhalika, Mhe Hasunga Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuchangia fedha hizo.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli haina dhamira ya kuwadunisha na kuwafedhehesha wananchi badala yake imejipambanua kuwanufaisha wakulima katika kilimo.

Alisema kuwa serikali imeamua kuwalipa fedha hizo wakulima ili kuendelea na uzalishaji bora wa mazao ya kilimo lakini kesi itakapomalizika serikali itazidai fedha hizo.

Mhe Hasunga amemuagiza Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Rukwa kupanga vizuri madai ya wakulima hao huku akisisitiza kutoingizwa majina mapya (Majina Hewa) yasiyohusika na madai ya fedha hizo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe Joachim Wangabo amempongeza Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kwa kukubali kulivalia njuga jambo hilo kwa kuwalipa fedha hizo wakulima kwani kufanya hivyo kutarahisisha wakulima hao kuendelea na uzalishaji wa mazao katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020.

Amesema kuwa maamuzi hayo ya wizara kuamua kuwalipa wakulima huku taratibu zingine za kisheria ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua Mwenyekiti huyo zikiwa zinaendelea zimeibua ari na nguvu mpya katika kilimo.

Awali, akisoma taarifa ya malalamiko ya kutapeliwa fedha hizo katibu wa chama cha MUZIA AMCOS Ndg Geofrey Mbati amesema kuwa pamoja na kupeleka malalamiko katika maeneo mengi lakini ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa ushirikiano wa karibu katika kipindi chote cha kutafuta muarobaini wa malipo ya wakulima.

Alisema kuwa miongoni mwa maoni ya wakulima ilikuwa ni ombi la kupatiwa fedha hizo kwa ajili ya kuwanusuru kutokana na kadhia hiyo ya muda mrefu iliyopelekea kushindwa kulipa ada za wanafunzi shuleni, kushindwa kuwekeza tena kwenye kilimo pamoja na kushindwa kumudu gharama za maisha hali iliyopelekea kuishi maisha ya kifukara.

No comments:

Post a Comment