TATIZO LA MAJI NANDAGALA LAWA HISTORIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 4 June 2019

TATIZO LA MAJI NANDAGALA LAWA HISTORIA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua maji baada ya kukabidhiwa kisima cha maji cha kijiji cha Nandagala ‘B’ kilichojengwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uturuki nchini Juni 3, 2019.  Kulia ni Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya jamii nchini, Muhammed Cicek na kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Turkish Maarif Foundation, Oguz Hamza Yilmaz. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

CHANGAMOTO ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama iliyokuwa inawakabili wananchi wa vijiji vya Nandagala ‘B’ na Ingawali wilayani Ruangwa imekuwa historia baada ya Ubalozi wa Uturiki kupitia taasisi yake ya Diyanet kuwachimbia visima virefu.

Visima hivyo viwili vimekabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Juni 3, 2019 na Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya jamii nchini, Muhammed Cicek. Hafla hiyo imefanyika katika kijiji cha Nandagala ‘B’. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania na Uturuki ni nchi rafiki na kwamba Serikali ya Uturuki imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Tanzania katika uboreshaji wa huduma za jamii zikiwemo za afya, elimu na maji.

Waziri Mkuu baada ya kuvipokea visima hivyo amewataka wananchi wa vijiji hivyo kupitia kamati zao za maji zihakikishe zinaisimamia vizuri miradi hiyo na pia wawe wanatoa taarifa za mapato na matumizi ya kila mwezi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Ruangwa, Samwel Pyuza ahakikishe huduma ya umeme inafikishwa katika mradi huo kwa ajili ya kusukuma maji badala ya kutumia jenereta.

Kwa upande wake, Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala za jamii nchini, Muhammed Cicek amesema Watanzania na Waturuki ni ndugu, hivyo amefurahi baada ya wananchi wa vijiji hivyo kupokea zawadi ya visima hivyo walivyowakabidhi.

Wakizungumza baada ya makabidhiano hayo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nandagala ‘B’ wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu na makazi yao.

Mmoja wa wakazi hao Safina Angulupele (63) amesema awali kabla ya kisima hicho walikuwa wanapata maji kutoka katika kijiji kingine na pia hayakuwa na uhakika, hivyo uwepo wa kisima kwenye kijiji chao ni mkombozi kwao.

Naye mkazi mwingine wa kijiji hicho Zainab Issa amesema huduma ya maji safi na salama ni muhimu kwa maendeleo ya jamii, hivyo anaipongeza Serikali kwa kuwafikishia huduma karibu na makazi. “Sasa hata sisi wazee tunaweza kwenda kisimani na kuchota maji.”

Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, imedhamiria kuwafikishia wananchi wote huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Attachments area

No comments:

Post a Comment