Muonekano wa Daraja la Sukuma lenye urefu wa Mita 100 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.3, ambalo ujenzi wake unaendelea. |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa aweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Daraja la Sukuma lenye urefu wa Mita 70 na barabara unganishi Kilometa 2.3 na kusisitiza kuwa Serikali ipo imara na inaendelea kuwahudumia watanzania na kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinawafikia watanzania wote.
Akizungumza Desemba 21, 2024 katika kjjiji cha Ngh’aya, wilayani Magu mkoani Mwanza, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo, Majaliwa amesema kuwa ujenzi unaenda vizuri na kuwahakikishia wananchi kuwa mradi huo utakuwa mkombozi kwa watu wa Magu na wilaya za jirani.
“Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika kwa kupelekewa huduma muhimu katika eneo lake ikiwemo barabara, madaraja, zahanati na shule”, amesema Majaliwa.
Aidha, Majaliwa ameeleza kuwa Utekelezaji wa miradi hiyo unaonesha namna Serikali inavyofanya kazi kwa kuleta maendeleo nchini.
Katika hatua nyingine Majaliwa amekagua ujenzi wa daraja la Simiyu lenye urefu wa mita 175 na barabara unganishi yenye urefu wa Kilometa 3 ambapo amesema kuwa Serikali imeona umuhimu wa kujenga daraja hilo ambalo lilijengwa tangu enzi ya mkoloni na kuamua kulijenga upya na kuwa la kisasa.
Aidha, amewataka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema kuwa Ujenzi wa daraja hilo utasaidia kupunguza ajali kwa kiasi kikubwa kutokana na kwamba daraja la zamani lilikuwa na njia moja ila la sasa litakuwa na njia mbili.
Ameongeza kuwa Ujenzi wa madaraja hayo ni moja ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kuboresha sekta ya miundombinu nchini ambapo daraja la Sukuma limefika asimia 24 na Simiyu limefika asilimia 35 ambayo yote yanagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Amefafanua kuwa kukamilika kwa madaraja hayo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kukuza na kuchochea uzalishaji katika sekta za kilimo, madini na viwanda.
Waziri Mkuu amefanya ziara ya ukaguzi na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali mkoani Mwanza ikiwemo ujenzi wa daraja la Sukuma na Simiyu ambayo yanagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi
No comments:
Post a Comment